WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewasimamisha kazi
vigogo 16 wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa tuhuma za ufisadi.
Idadi hiyo inafanya waliosimamishwa kazi katika bandari hiyo hadi sasa kufikia 23.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akizungumza na wafanyakazi wa
mamlaka ya Babdari (TPA)jana kuhusu uwajibikaji katika kuleta mabadiliko
sehemu ya kazi.
Akizungumza na wafanyakazi wa TPA Dar es Salaam
jana, Dk Mwakyembe alisema vigogo hao wamesimamishwa kazi kutokana na
tuhuma mbalimbali.
“ Bodi imewasimamisha kazi kutokana na tuhuma
mbalimbali za wizi na migongano ya kimaslahi, hawa wamesimamishwa baada
ya bodi kuichambua ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na tume niliyoiunda,”
alisema.
Waliosimamishwa kazi na nyadhifa zao kwenye mabano
ni Bakari Kilo (Mkurugenzi Uhandisi), Raymond Swai (Meneja Uhandisi),
Frolence Nkya (Mkurugenzi wa Mipango) na Mahebe Machibya (Meneja Ununuzi
na Ugavi).
Wengine ni Teophil Kimaro (Meneja Ununuzi), Mary
Mhayaya (Afisa Uhandisi Mkuu), Ayoub Kamti (Mkurugenzi wa Tehama),
Mathew Antony (Meneja Kitengo cha Kontena) Maimuna Mrisho (Mkurugenzi wa
Mifumo wa Menejimenti).
Wengine ni Fortunatus Sandalia (Askari kitengo cha
Ulinzi), Fadhili Ngolongo (Kitengo cha Marine), Mathew Antony (Meneja
Kontena), Mohamed Abdullah (Kitengo cha Mafuta), Kilimba (Idara ya
ulinzi) na Owen Rwebu.
Mwakyembe alisema katika ripoti ya uchunguzi imegundulika kwamba baadhi ya vigogo wa Bandari wanamiliki kampuni ambazo zinafanya kazi za TPA.
“Tumebaini kuwa kuna mgongano mkubwa wa kimaslahi
ndani ya bandari, kuna wafanyakazi wengine wana kampuni za mkononi
ambazo hazijasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela)
lakini zimepewa kazi za TPA,” alisema.
Alisema kampuni hizo zinapomaliza muda wa mikataba yao huongezewa muda wa mikataba mingine.
Dk Mwakyembe alisema kuna mtandao mkubwa
unaofanywa kwa watu mbalimbali kwa kushirikiana na vigogo wa bandari ili
kufanikisha wizi katika bandari.
“Kontena zinayeyuka, zinaibwa kama Twiga
walivyopandishwa kwenye ndege, ninaapa mtandao huu nitaumaliza hapa
bandarini,” alisema Mwakyembe huku akishangiliwa na wafanyakazi.
CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI.
CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment