MSANII Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, ameepuka adhabu ya
kunyongwa hadi kufa kwa tuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba
baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumbadilishia mashtaka, ambapo
sasa anatuhumiwa kuua bila kukusudia.
Kutokana na mabadiliko hayo, Lulu ameepuka adhabu
hiyo kwani hata kama atapatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo cha
maisha au kuachiwa huru.
Hii inatokana na kifungu cha 196 cha kanuni za adhabu ya kosa la kuua bila kukusudia, ambapo anayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha, miaka kadhaa au kuachiwa huru.
Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliliambia
gazeti hili kwamba uzoefu wa adhabu nyingi za kuua pasipo kukusudia
zilizowahi kutolewa nchini, ni kati ya miaka 15 na wengine waliachiwa
huru.
Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba Aprili 7, 2012.
Hata hivyo, jana upande wa mashtaka ulieleza
mahakamani kuwa kwa sasa imebadilisha mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia
na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha CP.
Mshtakiwa huyo alitarajiwa kusomewa mashtaka hayo
mapya jana pamoja na maelezo yote ya kesi, ambapo angesomewa ushahidi wa
mashahidi wote pamoja na vielelezo muhimu katika kesi hiyo.
Hata hivyo, hatua hiyo ilikwama kutokana na Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka anayeiendesha kesi hiyo
kutokuwapo mahakamani na badala yake aliwakilishwa na Wakili wa
Serikali, Ofmedy Mtenga.
“Upelelezi wa shauri lako umeshakamilika na tungeweza kukusomea comital (maelezo ya kesi) leo, lakini kwa kuwa waendesha mashtaka hawapo basi tunaliahirisha mpaka tarehe nyingine.”, alisema Hakimu Mkazi Agustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali.
Taarifa hizo za kukamilika kwa ushahidi wa kesi hiyo zilipokewa kwa furaha na shangwe na msanii huyo, kiasi kwamba alishindwa kujizuia kuonyesha furaha yake.
Wakili wake Peter Kibatala aliiomba mahakama itoe
ahirisho fupi hadi Ijumaa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa mashtaka haya
mapya pamoja na maelezo ya awali.
Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.
CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LWA MWANANCHI.
Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.
CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LWA MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment