WATU
wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia gari lililokuwa linasafirisha
maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani Mara kisha kupora takriban
Sh19.8 milioni walizokuwa nazo waombolezaji.
Katika
tukio hilo la kusikitisha lililotokea juzi mkoani Singida, majambazi
hao walivunja vioo vyote vya gari pamoja na jeneza lililokuwa na mwili
wa Munchari Lyoba aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo
Kikuu cha Sokoine (SUA) cha Morogoro na kumpekua marehemu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana nje ya chumba cha kuhifadhi maiti cha
Hospitali ya Mkoa wa Singida, mkuu wa msafara uliokuwa ukisafirisha
maiti, Makaranga alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 usiku
katika gari aina ya Land Cruiser mali ya SUA.
Akisimulia
tukio hilo, Makaranga alisema kuwa lilitokea katika Barabara Kuu ya
Dodoma – Mwanza nje kidogo ya Mji wa Singida kwenye kona maarufu kwa
jina la Mohammed Trans kuelekea mkoani Mara.
Alisema
kuwa gari hilo pamoja na jeneza, lililobeba viongozi wa wanafunzi sita
na viongozi wengine wanne lilipofika eneo la tukio, walikuta mawe
makubwa yamepangwa barabarani na kuwalazimisha kusimama ndipo wakavamiwa
na kundi kubwa la vijana, ambao walibeba bunduki mbili aina ya gobore,
marungu, mashoka na mawe.
“Walipofika
walipiga kioo cha gari letu kwa mbele na kumparaza kwa panga usoni
dereva wetu. Baada ya hapo walivunja vioo vyote na kutuamuru kutoa kila
kitu tulichokuwa nacho,” alisema Makaranga.
Makaranga
alisema kuwa katika tukio hilo, aliporwa Sh2 milioni alizokabidhiwa
azihifadhi kwa ajili ya kugharimia msafara huo, Sh8.8 milioni
zilizochangwa na wanafunzi kama rambirambi kwa mwenzao na jumla ya Sh9
milioni ambazo wasindikizaji walikuwa nazo mifukoni mwao.
“Pia tuliporwa simu zetu zote za mikononi, viatu, laptop na mabegi yote ya nguo zetu,” alisema.
Makaranga
aliyeeleza kuwa anafanya kazi za kiutawala SUA, aliwataja walioumizwa
na majambazi hao kuwa ni pamoja na yeye, dereva wao na kiongozi wa
wanafunzi, Idd Idd ambao walitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida
na kuruhusiwa.
Mkuu
wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kueleza kuwa amewasiliana na uongozi wa SUA ili watume
gari lingine na kukarabati jeneza lililoharibiwa na majambazi hao.
Mlozi
aliongeza kuwa kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Kamati ya Ulinzi
na Usalama, watahakikisha watu waliofanya unyama huo, wanakamatwa haraka
iwezekanavyo ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
“Nimesikitishwa
sana na tukio hili, inaelekea sasa binadamu tunaanza kutoka kwenye utu
na kuhamia kwenye vitendo ambavyo binadamu wa Mwenyezi Mungu hawezi
kuthubutu kuvifanya. Watu wanafikia hata kufungua jeneza na kuanza
kulisachi,” alisema Mlozi akionyesha masikitiko.
Chanzo: mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment