TIMU ya soka ya Tanzania bara ‘Kilimanjaro Stars’, leo inashuka
dimbani kuwania tiketi ya fainali ya Kombe la Chalenji dhidi ya wenyeji
na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Uganda Cranes.
Wakati Bara ikitinga hatua hiyo kwa kuwang’oa Rwanda kwa mabao 2-0,
Uganda wametokea kuwatupa nje ya michuano hiyo Ethiopia kwa kuwatungua
bao 2-0.
Ni mechi inayotarajiwa kuwa yenye mvuto na ushindani mkubwa kutokana na
rekodi ya timu hizo mbili, kwani Stars itashuka dimbani ikikumbuka
kipigo cha mabao 3-1 zilipokutana kwenye hatua hiyo mwaka jana kwenye
Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Uganda baadae iliifunga Rwanda
kwa penalti 3-2 katika fainali baada ya kumaliza dakika 120 kwa sare ya
2-2.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Stars, Kim Poulsen amewasihi waamuzi
kutenda haki hasa wakizingatia watakuwa wakicheza na bingwa mtetezi
anayecheza nyumbani.
Wakati Uganda ikitaka kushinda ili kutinga fainali itakayochezwa Desemba
8 na kutetea taji lake, pia kuweka rekodi ya kulibeba mara 13 tangu
1973, Stars wanajaribu kuubeba ubingwa huo mara ya nne.
Akizungumza baada ya mazoezi ya jana kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu
Kyambogo, Poulsen alisema kwa kutambua yote hayo, timu yake
inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia ya
Kilimanjaro Premium Lager, vijana wake watapambana kushinda kutinga
fainali.
“Vijana wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya
kucheza ila tunachoomba ni ‘fair play’ kutoka kwa mwamuzi maana
tunacheza na wenyeji ambao wana watazamaji wengi,” alisema Poulsen.
Alisema timu zote mbili ni nzuri na kama mwamuzi atachezesha vizuri kwa haki, basi itakuwa ni mechi ya kuvutia.
“Vijana wana ari na mechi na kukiwa na ‘fair play’ tutacheza vizuri kama tulivyofanya dhidi ya Rwanda,” alisema Poulsen.
Mwamuzi wa mechi hiyo ni Mohamed El Fadil kutoka Sudan aliyechezesha mechi ya robo fainali kati ya Stars dhidi ya Rwanda.
Alisema faraja kwake ni kutokuwa na majeruhi huku akiwasifu nyota wake
kwa kuonesha uwezo, nidhamu na mshikamano mkubwa akisema vitu hivyo ni
muhimu kwa timu inayopigania ushindi.
“Hawa wanakaa kama familia, si unawaona walivyo pamoja?” alisema Poulsen na kuongeza kuwa, hilo ni muhimu sana kwa mchezaji.
Naye kocha msaidizi, Marsh Sylvester alisema Stars inayo nafasi kubwa ya
kushinda mechi hii kutokana na wenyeji wao kusumbuliwa na presha ya
mashabiki wao.
“Timu yetu iko ‘motivated’ kabisa na ukizingatia Uganda wako nyumbani,
wao ndio wana ‘tension’ kubwa zaidi,” alisema na kuongeza kuwa mchezo
huu utakuwa wa kusisimua sana.
Akizungumzia mechi ya leo kutoka Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya
Kilimanjaro, George Kavishe alisema Stars ina kila sababu ya kushinda na
kutinga fainali kisha kutwaa ubingwa wa nne.
Mechi hiyo ya Stars na Uganda, itatanguliwa nyingine kati ya Zanzibar
dhidi ya Kenya, inayaotarajiwa kuwa yenye ushindani mkubwa.
Kocha wa Zanzibar, Salum Nassor ametamka mara mbili kwamba kama Zanzibar
itashindwa kuondoka na ubingwa, hataona sababu ya kuendelea kuinoa timu
hiyo.
Mechi ya fainali na mshindi wa tatu wa michuano hiyo, zote zitachezwa
Jumamosi ambapo bingwa ataondoka na kitita cha dola 30,000; mshindi wa
pili dola 20,000 huku mshindi wa tatu akilamba dola 10,000 za Marekani.
No comments:
Post a Comment