BAADA ya klabu ya Simba kulaani kitendo cha Azam FC kumuuza
mchezaji Mrisho Ngassa kwa El Mereikh ya Sudan, klabu hiyo sasa umeamua
kushtaki suala hilo kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF).
Juzi, Azam FC ilitangaza kumuuza Ngassa kwa dola 75,000 huku ikipanga
kumpatia dola 50,000 kama dau la kusaini mkataba wa miaka miwili.Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, Azam wamefanya
uhuni katika mazingira ya kumuuza Ngassa kwani nyota huyo ana mkataba na
Simba utakaokwisha Mei 31, 2013.
Alisema kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo kwenye mkataba wa Ngassa, Simba na Azam zote zina mamlaka na mchezaji huyo, hivyo hakuna mmojawapo kufanya maamuzi bila kumshirikisha mwingine.
“Mkumbuke mbali ya dola 25,000 tulizotoa kwa Azam FC, tuliingia
gharama nyingine za kumshawishi zaidi kama gari, donge nono, pia tulimpa
kazi ya ziada kocha wetu kuhakikisha anapandisha kiwango cha Ngassa,”
alisema.
Kamwaga alisema Azam wanajichanganya juu ya suala hilo kwani awali
waliandika barua kuwa Ngassa amepata timu, hivyo anataka kuondoka Simba
kabla ya kuandika barua nyingine kuwa wameamua kumuuza kwa sababu Simba
imemsainisha mkataba mwingine.
“Kwa hali hii inaonesha jinsi gani Azam wanavyotapatapa…sisi
hatujamsainisha mkataba mpya na kama wana uhakika huo waulete, ukweli ni
kwamba mkataba wetu na Ngassa ni kuichezea Simba hadi Mei 31 na baada
ya hapo kama atataka rurejea Azam, kubaki Simba au kwenda timu nyingine
ataamua,” alisema.
Kamwaga aliongeza kuwa hawatakuwa tayari kumpoteza nyota huyo kirahisi
na tayari wamendika barua TFF kuitaka kutotoa hati ya uhamisho wa
kimataifa (ITC) kwa El Mereikh.
“Pia tumeishtaki Azam TFF kwa kukiuka sheria 17 za soka kwani kitendo
hicho si cha kiungwana na kinapaswa kukemewa kwa nguvu zote,” alisema.
Naye mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, na mwenyekiti wa
kamati ya usajili, Zakaria Hanspope, wamewasili nchini Uganda kufuatilia
baadhi ya mambo ikiwemo kuteta na Ngassa juu ya suala hilo.
Kamwaga alisema viongozi hao pia watafuatilia suala la kocha hivyo
wakiwa huko, watazungumza na Kocha Kinnah Phiri wa timu ya taifa ya
Malawi.
“Wamekwenda huko wakiwa wamekamilika kwani hata masuala ya Okwi yatamalizwa hukohuko na mengineyo mengi,” aliongeza Kamwaga.
No comments:
Post a Comment