KAMPUNI ya Rena Events imetangaza zawadi zenye thamani ya sh
mil. 100 zitatolewa kwa washindi wa shindano la mwaka huu la Miss East
Africa litakalofanyika Desemba 21 kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Rena Events, Rena Callist
alisema mshindi atapata zawadi zenye thamani ya dola 30,000 za Marekani,
ikiwemo gari aina ya Mazda lenye thamani ya dola 15,000 za Marekani.
Mbali ya zawadi hizo, pia mshindi wa kwanza atapewa mkataba wa kufanya
kazi na Miss East Africa Organization wenye thamani ya dola 15,000 za
Marekani.
Calist alisema mshindi wa pili atapata zawadi zenye thamani ya dola
8,000 za Marekani na fedha taslimu dola 2,000, na mkataba wa kufanya
kazi na Kamati ya Miss East Africa wenye thamani ya dola 6,000.
Aidha, mshindi wa tatu atapata zawadi zenye thamani ya dola 5,000,
fedha taslimu dola 1,500 na mkataba wa kufanya kazi na Kamati ya Miss
East Africa ambao utakuwa na thamani ya dola 3,500.
Katika hatua nyingine, Calist amefafanua kuwa sababu kubwa ya shindano
hilo kusogezwa hadi Desemba 21, ni kutoa fursa kwa warembo na waandaaji
kujipanga zaidi kwani lengo ni kufanya shindano hilo kuwa bora
kulingana na hadhi yake.
Shindano hilo litashindanisha warembo kutoka Tanzania, Kenya, Uganda,
Rwanda, Burundi, Somalia, Djibouti, Eritrea, Sudan, Ethiopia, Malawi,
Seychelles, Sudan Kusini na wengine ambao wanaishi nje ya Afrika kama
Ubelgiji, Ufaransa na Uholanzi.
Kwa upande wa wadhamini, Calist aliwataja Hifadhi ya Taifa ya
Ngorongoro, TANAPA, Ethiopian Airlines, DTP, Ako Catering, Darlings
Hair, Seascape Hotel, Satguru na Clouds FM.
No comments:
Post a Comment