WALIMU
wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Ruaruke wilayani Rufiji, Mkoa wa
Pwani, wameitelekeza shule hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya
baadhi ya wanafunzi kuwadhalilisha kimapenzi, ikiwamo kuwabaka baadhi
yao.
Habari
zilizolifikia gazeti la Mwanachi jana zimeeleza kuwa mbali na
udhalilishaji huo, wanafunzi hao wamekuwa wakiwatishia maisha walimu wao
kwa namna mbalimbali. Katika moja ya vitisho hivyo, wamechoma moto
nyumba zao tatu.Habari hizo zimeeleza kwamba walimu hao wamelazimika kuikimbia shule
hiyo baada ya baadhi ya walimu wa kike kutongozwa na wanafunzi, kupigwa
mabusu kwa nguvu hadharani, kutishiwa kuchomwa visu na kuchorwa vikatuni
vya kudhalilisha.
Mmoja wa walimu hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini akihofia
kushughulikiwa na wanafunzi hao alisema amelazimika kuikimbia pamoja na
walimu wenzake wote, kwa kuwa wameshindwa kudhibiti tabia hiyo kutokana
na vijana hao kuungwa mkono na wazazi wao.
Akizungumza kwa simu akiwa Dar es Salaam, mwalimu huyo alisema shule
hiyo yenye wanafunzi 485, imepoteza mwelekeo, haitawaliki na mazingira
yake hayavutii walimu, hasa wa kike, kuishi na kufanya kazi.
“Tumevumilia vya kutosha, lakini kila kukicha hali inazidi kuwa mbaya.
Walimu wanafikia mahala wanabakwa! Kibaya zaidi wazazi na mamlaka
nyingine hazionyeshi ushirikiano kwetu, wazazi wanawa-support
(wanawaunga mkono) watoto wao,” alieleza.
Hata
hivyo, mwalimu huyo hakuwa tayari kueleza kwa undani kuhusu vitendo
hivyo vya ubakaji lakini alieleza kwamba vimekuwa vikitokea walimu hao
wanapokuwa katika matembezi usiku.
Vitendo hivyo vimekuwa vikitokea baada ya wanafunzi hao kuwatongoza walimu wao na kukataa kufanya nao mapenzi.
Mwalimu huyo alidai kuwa walimu wamekuwa wakitishiwa kuchomwa visu na
nyumba zao kuchomwa moto, huku walimu wanne wa kike wakidhalilishwa
kimapenzi kwa kupigwa mabusu na kutongozwa na wanafunzi.
“Wanafunzi
wamefanya mtihani wa kidato cha pili chini ya ulinzi wa askari polisi
wenye silaha kitu ambacho si cha kawaida,” aliongeza.
Alipoulizwa kuhusu
tukio hilo, Ofisa Elimu Sekondari, Adnan Mwenda alisema asingependa
kuzungumzia tatizo hilo kwa kuwa siyo msemaji. Akashauri atafutwe
mkurugenzi wa wilaya… “Unaweza kuzungumza mambo mengine yakakuletea
matatizo,” alisema Mwenda kabla ya kuelekeza atafutwe mkurugenzi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Leonard
Rwegasira alithibitisha walimu hao kuikimbia shule hiyo na kusema kuwa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, itakutana hivi karibuni kujadili
suala hilo.
“Ni kweli shule hiyo imetelekezwa, walimu wamekimbia na
wanafunzi hawaendi shule. Tatizo tunalifahamu na Mkuu wa Wilaya anafanya
jitihada mbalimbali kurekebisha tatizo hilo,’ alisema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruaruke, Hemedi Mpullu pia alithibitisha
walimu hao kuitelekeza shule hiyo na kusema Mkuu wa Wilaya ya Rufiji,
Nurdin Babu ameagiza kufanyika kwa kikao cha dharura ili kupatikana
mwafaka kati ya walimu hao, wanafunzi na wazazi.
“Mbunge wa Kibiti,
Abdul Marombwa amepanga pia kufanya mkutano hapa Ruaruke ili kutafuta
mwafaka,” alisema Mpullu.
Katibu
wa Chama Cha Walimu (CWT), Wilaya ya Rufiji, Manyama Lazaro alisema
kuondoka kwa walimu hao, kumefanya shule hiyo ijifunge yenyewe, kwani
wanafunzi nao sasa hawaendi shule.
“Wanafunzi wamefikia hatua ya kuwachora walimu wa kike wakifanya
mapenzi na walimu wa kiume katika kuta za vyoo! Huu ni udhalilishaji
mkubwa,” alisema.
Lazaro alieleza kuwa katika siku za hivi karibuni,
wanafunzi hao walichoma moto nyumba tatu za walimu na Bodi ya Shule
iliamua kuwa wanafunzi hao waitwe na wazazi wao ili walipe gharama za
uharibifu.
Chanzo: MWANACHI
No comments:
Post a Comment