Azam
FC jana imemuuza mchezaji wake Mrisho Halfan Ngasa kwa klabu ya El
Mereikh katika majadiliano yaliyochukua takriban saa moja kwenye makao
makuu ya klabu ya Azam FC na kuhudhuriwa na viongozi wa pande zote
mbili.
El-Mereik wameshazungumza na mchezaji na kukubaliana maslahi
yake binafsi ambapo Mrisho Ngasa atalazimika kusafiri hadi mjini
Khartoom Sudan mara baada ya kuisha mashindano ya CECAFA Challenge Cup
ili kuona mazingira ya klabu, kufanya vipimo vya Afya na kuangalia
makazi yake binafsi. Kuuzwa kwa Mrisho Ngasa nchini Sudan kunaifanya
klabu ya Azam FC kupata kiasi cha zaidi ya Dola 50,000 pesa ambayo Azam
FC waliiweka kama kima cha chini cha kumuuza Mrisho Ngasa.
Wakati
Azam FC ikimtoa Ngasa iliweka kiasi hicho cha dola 50,000 kwa timu
itakayomtaka lakini kutokana na kukosekana na mnunuzi huku Simba ikitoa
ofa ya shilingi milioni 25, Azam FC iliamua kumpeleka Ngasa kwa mkopo
ili akitokea mteja mwenye kufikia dau hilo waweze kumuuza.
Mengi
yalisemwa juu ya biashara ya mkopo kati ya Azam FC na Simba lakini
msimamo wa Azam FC uliowekwa kwenye tovuti hii leo umethibitika baada ya
El-Mereikh kufikia dau la kumnunua Mrisho Ngasa.
Mrisho Ngasa,
mchezaji mwenye kipaji cha hali ya Juu cha kusakata kabumbu anakwenda
nchini Sudan kwenye kikosi chenye mafanikio zaidi katika ukanda huu wa
Afrika Mashariki na kati baada ya TP Mazembe.
Azam FC inamuuza
Mrisho Ngasa kwa kuzingatia umuhimu wa maendeleo ya mchezaji mwenyewe
kimpira na kwa kipato, pia kwa kuzingatia kwamba Tanzania inahitaji
wachezaji wengi wanaocheza nje kwenye vilabu vikubwa ili wanaporudi
waweze kuisaidia timu ya Taifa.
No comments:
Post a Comment