HALI ya utendaji kazi katika kikosi cha zimamoto na uokoaji cha
Ilala jijini Dar es Salaam, imezidi kuwa mbaya baada ya magari mawili
yaliyokuwa yakitegemewa kufanya kazi kuharibika na kushindwa kufika
kwenye matukio ya uokoaji.
Magari yaliyokuwa yakifanya kazi hadi juzi yalikuwa ni benzi lenye
namba STK 1066 na STH 3856 aina ya Scania, ambayo yalishindwa kufika
katika matukio ya moto uliotokea juzi eneo la Biafra na Mbagala Mbande,
jirani na uwanja wa Azam, huku tukio lingine likiwa ni lile la jana
asubuhi katika moja ya majengo ya usalama wa taifa Makumbusho.
Mbali ya magari hayo kuwa mabovu pia mawasiliano ya simu ya dharura
ndani ya kikosi hicho ni ya kutia shaka, baada ya simu mbili kati ya
tatu zilizokuwa zikitumika kupokelea taarifa za dharura kuharibika huku
ile iliyobakia ufanyaji kazi wake ukiwa hauna uhakika.
Wakizungumza wafanyakazi wa jeshi hilo walisema taarifa za ubovu wa magari
hayo wameshazifikisha kwa viongozi wao huku kukiwa hakuna jitihada za
kushughulikiwa.
“Haya magari ni ya kanda ya Ilala ila yanatumika kwa ajili ya huduma
kwa jiji zima kwa kuwa kanda zingine hazina magari na sasa yameharibika,
unavyoyaona hapo hayana breki, ving’ora na vimuli-muli,” alisema mmoja
wa wafanyakazi hao.
Aliongeza kuwa licha ya kutoa taarifa kwa uongozi juu ya ubovu wa
magari hayo na vifaa vingine, wamekuwa wakilazimishwa wayatumie hivyo
hivyo hali iliyosababisha moja ya magari hayo kutaka kugonga magari
mengine kwa sababu ya kukosa breki wakati likijaribiwa kama linaweza
kufanya kazi.
Mfanyakazi mwingine alisema hali hiyo ya ubovu wa vifaa haishii kwenye
magari peke yake na kueleza kuwa hata simu ya ofisi kwa sasa haina
uhakika wa kupatikana hewani na kuwafanya wafanyakazi wa kikosi hicho
kutumia muda mwingi kupumzika katika vyumba vyao pasipo kufanya kazi.
“Hakuna umakini na uwajibikaji kwa viongozi wetu juu ya vifaa kwa
maana hata tunapolala ni sehemu ya hatari kiafya magodoro yameisha,
yananyofoka na hayana foronya huku viongozi wetu wakiwa wanakusanya
fedha na kwenda kukaa vikao vya kupanga matumizi yatakayowanufaisha
wao,” alisema mfanyakazi huyo.
Kamanda wa kikosi cha uokoaji na zimamoto mkoa wa Ilala (RFO) Athuman
Nassa alipotakiwa kutolea ufafanuzi taarifa hizo alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo kwenye simu na kumtaka mwandisahi apange siku
wakutane.
No comments:
Post a Comment