WATETEZI wa Haki za Binadamu wanaofanya shughuli zao katika
maeneo ya migodi wametakiwa kutorudi nyuma katika kutetea haki za
wanyonge kutokana na vitisho ambavyo wamekuwa wakipata wakati wa
kufuatilia taarifa mbalimbali maeneo hayo.
Wito huo ulitolewa na Mratibu wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu
(THRD-Coalition), Onesmo Olengurumwa, wakati wa uzinduzi wa ripoti
inayoonyesha namna watetezi hao wanavyofanyiwa vitendo vya
udhalilishwaji wanapohitaji taarifa katika migodi mbalimbali iliyopewa
jina la ‘Only the Brave Talk About Oli’.
Olengurumwa alisema kutokana na kukabiliwa na hatari hiyo wamekuwa
wakikutana mara kwa mara ili kupeana mbinu za namna ya kupata taarifa
bila kudhurika.
Alisema ni muhimu jamii ifaidike na uchimbaji wa raslimali hiyo kwa
kuwa ni haki yao Kikatiba hivyo wana wajibu wa kuzitetea, kuzifuatilia
na kutoa maoni yao ya namna gani zitumike.
Naye Balozi Msaidizi wa nchi ya Sweden, Maria Van Berlekon, alisema
changamoto ambazo zimekuwa zikiorodheshwa mara kwa mara na Watetezi wa
Haki za Binadamu hapa nchini ni za ukweli na sio za kufikirika.
Van Berlekon ambaye nchi yake imedhamini uandaaji wa ripoti hiyo,
alisema wangependa kuona fursa zilizopo katika migodi mbalimbali
zinawafaidisha Watanzania na kuwepo kwa uwazi hasa katika suala zima la
uingiaji wa mikataba.
No comments:
Post a Comment