Cote D'Ivoire, kwa msaada mkubwa wa Togo imefanikiwa kufuzu kuingia
katika duru ya robo fainali za mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika
Jumamosi(26.01.2013) wakati Algeria ikitupwa nje ya mashindano hayo.
Siku ya nane ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika iifanyika huko
Rustenburg, ambako Tembo wa Cote D'Ivoire wakitokea kutoka katika
kuonyesha mchezo dhaifu wakati wa michezo ya ufunguzi na kuonyesha ubabe
wake dhidi ya Tunisia kwa kuibamiza mabao 3-0, magoli yakifungwa na
Gervinho, mchezaji mwenzake katika ligi ya Uingereza Yaya Toure , na pia
mchezaji wa akiba aliyeingia dakika za mwisho Didier Ya Konan.
Wakati Togo ilipoishangaza mabingwa wa zamani wa kombe hilo Algeria kwa
kuichapa mabao 2-0 katika mchezo wa pili, Cote D'Ivoire walihakikishiwa
nafasi ya kwanza katika kundi D, bila kujali matokeo ambayo yatatokea
wakati pazia litakapofungwa katika duru ya kwanza ya ligi hiyo ndogo
Jumatano wiki ijayo katika kundi hilo.
Pambano kati ya Algeria na Togo 0:2
Togo , ambayo ilijipatia mabao yake kupitia mshambuliaji wa Tottenham
Hot Spurs Emmanuel Adebayor na mchezaji wa akiba Dove Wome, ilipata
ushindi wa kushtua dhidi ya Algeria , na sasa inahitaji tu sare dhidi ya
Tunisia kuweza kuchukua nafasi ya pili katika kundi hilo na kutinga
katika robo fainali.
Algeria na Tunisia vichwa chini
Wakati timu hizo mbili zikisherehekea kazi nzuri walizofanya, hali
ilikuwa ya fadhaa katika kambi ya Algeria , timu yenye wachezaji wenye
vipaji lakini hawana uzoefu.
Wachezaji wa Togo wakishangiria ushindi wao wa bao 0:2
Kocha Vahid Halilhodzic aliwasili katika mkutano wa kawaida wa baada ya
mchezo na waandishi habari akionekana kuwa katika hali ya masikitiko
makubwa , kama vile mtu aliyeshinda fedha nyingi katika bahati nasibu,
lakini akagundua kuwa mbwa amekula tikiti yake iliyoshinda.
"Ni maafa makubwa, " amesema.
"Najihisi aibu kubwa. Sijui kile kilichotokea leo, ni vigumu kufanya tathmini.
"Pengine wachezaji hawajakuwa wapevu vya kutosha kushiriki katika kiwango hiki.
"Lakini sitamshutumu yeyote, nilifanya uchaguzi. Ninajihisi tu aibu.
"Hali yangu ya baadaye kama kocha haina umuhimu, kile chenye umuhimu ni
kwamba tunajaribu kuangalia juu ya vipi tunaweza kucheza kiwango kile
cha mchezo na kisha tunashindwa.
Ameongeza: "Inaeleweka mashabiki wamekasirika, walikuwa na matarajio makubwa."
Togo, ambayo ilibakiza dakika mbili tu kuweza kuidhibiti Cote D'Ivoire
katika mchezo wao wa ufunguzi, ilifanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza
katika mashindano haya ya kombe la mataifa ya Afrika tangu pale
walipoweza kuishinda Cameroon miaka 13 iliyopita.
Adebayor ambaye alikubali kujiunga na timu hiyo baada ya mvutano wa muda
mrefu juu ya malipo ya bonasi , usalama na hali ya soka nchini Togo,
alionekana mwenye furaha wakati alipojitokeza mbele ya waandishi habari.
"Tulicheza vizuri dhidi ya Cote D'Ivoire , lakini kwa bahati mbaya ,
hatukushinda. Tumekuja pamoja na kusonga mbele na hii inaonesha kuwa
iwapo kila mtu atajiunga pamoja tunaweza kupata mafanikio makubwa."
Kocha Didier Six hakutafuna maneno: "Tulipambana na timu nzuri sana ya
Algeria, tulistahili kushinda. Togo ilikuwa na nia ya ushindi."
Adebayor ambaye alijificha chini ya kiti cha basi wakati timu yao
iliposhambuliwa kwa risasi kabla ya fainali za mwaka 2010 nchini Angola
na watu wawili wakafariki, aliongeza: "Ni muhimu kila wakati kufunga
katika fainali za kombe la Afrika. Tulijua kuwa tunahitaji kushinda
baada ya kushindwa katika mchezo wa kwanza. Tulishambulia vizuri, na
kutumia nafasi zetu tulizozipata. Na sasa natumai kutakuwa na sababu
nyingi za kufurahi.
Drogba apumzishwa
Hapo mapema , kocha wa Cote D'Ivoire Sabri Lamouchi alitoa kali, kwa
kumuacha nje nahodha Didier Drogba wakati akizungusha kikosi chake kutoa
nafasi kwa wengine.
Nahodha wa Cote D'Ivoire Didier Drogba
Duru ya mwisho
Wakati duru ya mwisho ya michezo ya makundi ya kombe la mataifa ya
Afrika ikianza leo Jumapili (27.01.2013) kwa michezo ya kundi A, timu
kadha bado zinanafasi ya kufuzu kuingia katika duru ya robo fainali,
katika fainali hizi za 29 za michuano ya bara ka Afrika.
Kundi A linaongozwa na Afrika kusini , Bafana Bafana , wakati wenyeji
hao wa mashindano wakiwa na points 4, Morocco na Cape Verde zikiwa na
points mbili kila moja na Angola ikiwa na point moja.
Iwapo Afrika kusini itaishinda Morocco mjini Durban , timu ngeni katika
mashindano haya Cape Verde itahitajika kupata sare tu dhidi ya Angola
kujihakikishia kusonga mbele.
Bafana Bafana wanaongoza kundi lao la A
Iwapo Bafana Bafana itatoka sare na simba hao wa milima ya Atlas
Morocco, Cape Verde inaweza kuchukua uongozi wa kundi hilo ikiwa itapata
ushindi dhidi ya Paa weusi wa Angola, ambao wenyewe wanaweza pia
kuingia katika duru ya robo fainali iwapo watawapa kipigo "papa wa
buluu" , Cape Verde, na kuwafungasha virago Morocco na Cape Verde.
Mambo yanaweza kuwa katika hali ya utata zaidi iwapo Afrika Kusini
Bafana Bafana itashindwa dhidi ya Morocco, nani anaweza kuwa na uhakika
wa kuingia katika robo fainali ni ushindi tu wa Cape Verde utakaoweza
kuizuwia Bafana Bafana.
No comments:
Post a Comment