Wanadamanaji wanaopinga uamuzi
Watu 22 wameuwawa (26.01.2013) katika mapambano ya kupinga kuhukumiwa
kwa adhabu ya kifo kwa watu 21 kutokana na kuhusika kwao katika ghasia
za soka zilizosababisha vifo vya watu 74 wakati wa mechi ya soka mwaka
jana
Watu sabini na tatu wakiwemo maafisa wa michezo na polisi wanashtakiwa
kwa madai ya mauaji ya kudhamiria au uzembe kuhusiana na ghasia hizo
zilizotokea kwenye uwanja wa Port Said hapo mwezi wa Februari.
Ghasia hizo zilizuka kati ya mashabiki hasimu wa timu wenyeji wa pambano
hilo Al Masry na Al-Ahly wakati wa michuano ya ligi kuu na kusababisha
watu 74 kupoteza maisha yao.Hayo yalikuwa ni maafa makubwa kuhusiana na
mchezo wa mpira wa miguu kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi
cha zaidi ya muongo mmoja.
Polisi wawili ni miongoni mwa watu waliouwawa katika ghasia za Jumamosi
na kwa mujibu wa mkurugenzi wa afya katika mji wa Port Said watu zaidi
ya 200 wamejeruhiwa.
Washitakiwa wengine kuhukumiwa Machi
Hakimu wa mahakama amesema hukumu kwa washtakiwa wengine 52 waliobakia
itatolewa tarehe tisa mwezi wa Machi. Kutokana na sababu za usalama
takriban washtakiwa wote hawakuwako mahakamani mjini Cairo wakati hukumu
hiyo ilipotolewa.
Washtakiwa wote wana haki ya kukata rufaa na kati ya wale waliohukumiwa Jumamosi hakuna askari yoyote.
Mahakama ya Cairo iliotowa hukumu hiyo sasa imeikabishi kwa kiongozi wa
juu wa dini nchini humo kwa maoni ya mwisho.Utekelezaji wa hukumu za
adhabu za kifo nchini Misri lazima uidinishwe na Mufti Mkuu.
Katika mji wa Port Said kumezuka mapambano kati ya waandamanaji na
polisi. Mashabiki wa timu ya Al-Masry na familia za washtakiwa wanasema
kulikuwa na mkono wa kisiasa katika kesi hiyo.
Polisi ilitumia gesi ya kutowa machozi kutawanya waandamanaji ambao walijaribu kulivamia gereza wanakoshikiliwa washtakiwa.
Timu ya Al-Ahly yasherehekea hukumu
Washabiki wa Al Ahly wakishangilia
Hata hivyo mamia ya mashabiki wa timu ya Al-Ahly walisherehekea
hukumu hiyo kwa kuwasha fataki na kuimba nyimbo katika mitaa ya Cairo.
Kulikuweko na nderemo ndani na nje ya mahakama katika mji mkuu huo
wakati hukumu hiyo ikisomwa mahakamani.Wanawake walipiga
vigeregere,familia na jamaa za wahanga walikumbatina na kupiga mayowe ya
"Allahu Akbar".
Mapambano ya Port Said yamepelekea kuwekwa kwa wanajeshi katika mji huo kulinda taasisi muhimu za serikali na kurudisha usalama.
Vituo viwili vya polisi vilivamiwa na milio mizito ya risasi ilikuwa
inasikikika kutoka kitongoji cha Al Manakh.Magari ya kubebea wagonjwa
yamekuwa yakipeleka majeruhi hospitali na maduka na shughuli zote za
biashara zilifungwa wakati waandamanaji wakiunguza mipira
barabarani.Misikiti katika mji huo imekuwa ikitowa wito kwa watu
kujitolea damu.
Uamuzi huo umekuja masaa machache baada ya vikosi kuwekwa katika mji
wa karibu wa mwambao wa Suez kufuatia mapambano kati ya polisi na
waandamanaji wanaopinga serikali kusababisha vifo vya watu tisa.
Mapambano ya Suez ni mabaya kabisa katika wimbi la ghasia lililozuka
nchini kote Misri hapo Ijumaa wakati wa maadhimisho ya miaka miwili ya
vuguvgu lilimn'gowa madarakani rais wa zamani Hosni Mubarak.
Muungano wa Ukombozi wa Taifa ambao ni muungano mkuu wa upinzani wa
vyama na makundi ya vuguvugu wenye kupinga utawala wa Waislamu wa
itikadi kali nchini humo umetowa wito miongoni mwa mambo mengine kuundwa
kwa serikali ya ukombozi wa taifa venginevyo hautoshiriki katika
uchaguzi ujao wa bunge.
Rais Mohamed Mursi ametowa wito wa kuwepo kwa utulivu na kuahidi kwamba
serikali itawafikisha mbele ya sheria wale wenye kuvunja sheria za nchi
hiyo. Ametaka watu waheshimu misingi ya mapinduzi ya Misri na kutowa
maoni yao kwa uhuru na kwa amani.
No comments:
Post a Comment