JESHI la Polisi mkoani Morogoro, linatarajiwa kufanya bonanza
kwa ajili ya kuuaga mwaka 2012 na kuukaribishwa 2013 kwenye Bwalo la
Umwema lililoko mjini hapa, leo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Kituo cha
Polisi mkoani
Morogoro (OCS), Idd Ibrahim, alisema kuwa bonanza hilo
linatarajiwa kushirikisha familia za jeshi hilo na wadau mbalimbali,
ikiwemo waandishi wa habari.
“Katika bonanza hili la kuukaribisha mwaka 2013, kutatanguliwa na
michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu kati ya jeshi hilo na
waandishi wa habari wa mkoa wa Morogoro,” alisema Ibrahim.
Aidha alisema kuwa, michezo mingine ni pamoja na netiboli kati ya
askari wa kike na wake za askari, kukimbiza kuku na mingineyo, ambapo
imepangwa kufanyika asubuhi kwenye uwanja wa Jamhuri.
“Michezo hiyo tunatarajia kuifanya asubuhi huku ikiongozwa na Kamanda
wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile,” aliongeza.
Hata hivyo, mara baada ya kukamilika kwa michezo hiyo, kutafuatiwa na
tafrija fupi itakayofanyika Bwalo la Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
Umwema, mjini hapa.
No comments:
Post a Comment