MZUNGUKO wa lala salama Ligi Kuu Tanzania Bara, unatarajiwa
kuanza kutimua vumbi leo kwenye viwanja sita tofauti kwa timu 12 kati ya
14 kuumana.
Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mabingwa watetezi Simba
wataanza kampeni za kutetea taji lao ambalo wameliweka rehani kwa
mahasimu wao Yanga, kwa kuwakaribisha African Lyon.
Simba ambayo ilikuwa Muscat Oman kwa kambi ya wiki mbili, itashuka
dimbani leo ikiwa chini ya benchi jipya la ufundi, likiongozwa na Kocha
Mkuu, Mfaransa Patrick Liewig, akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na
Meneja Moses Basena.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema, Mwamuzi Israel Nkongo
ndiye atakayechezesha mechi hiyo.
Na huko Manungu Turiani mkoani Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar watawakaribisha vibonde wa ligi, maafande wa Polisi Morogoro.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime, akizungumzia ligi hiyo, alisema ana
imani timu yake kufanya vema katika hatua ya lala salama, kutokana na
maandalizi aliyoyafanya licha ya ligi kuonekana kuwa ngumu na ya
ushindani zaidi.
“Msimu huu ligi ina ushindani sana na ndio maana nilijipanga mapema na
kufanya maandalizi ya uhakika, pia michuano ya Mapinduzi Cup
ilinisaidia sana, licha ya kutolewa katika hatua ya makundi,” alisema
Mexime na kuongeza kuwa kazi itaanza leo dhidi ya maafande hao wa Polisi
Morogoro.
Naye Abdallah Kibadeni ‘King’ wa Kagera Sugar ambaye leo atakuwa Azam
Complex kuwavaa wenyeji Azam FC, alisema hawezi kuongea sana bali kazi
yake ni vitendo.
Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Chalres Kilinda, ambaye atakuwa na kibarua
dhidi ya ndugu zao Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi
Pwani, alisema uimara wa kikosi chake kwa sasa ni tofauti na mzunguko wa
kwanza ambapo hawakuweza kufanya vizuri.
Wagosi wa Kaya, Coastal Union, watakuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kulikabili gwaride la Mgambo JKT.
Kesho maafande wa Tanzania Prisons watashuka dimba la Taifa jijini Dar
es Salaam, kuwavaa vinara wa ligi hiyo, Yanga ambao wanarejea na kasi
mpya baada ya kambi ya wiki mbili nchini Uturuki.
Kocha wa Prisons ambao mechi ya kwanza walilazimisha sare ya bila
kufungana, Jumanne Chale, alisema, ana imani nyota kadhaa walioongezwa
katika dirisha dogo, wataisaidia timu yake, akiwemo mkongwe Emmanuel
Gabriel ‘Batigoal’ ambaye alitamba vilivyo na Wekundu wa Msimbazi enzi
zake.
No comments:
Post a Comment