HATIMA ya kuanza kwa raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara iliyopangwa
kuanza Januari 26, itajulikana leo katika kikao cha pamoja baina ya
serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu za Ligi Kuu
zilizotishia kutocheza bila kupewa fedha za nauli.
Novemba mwaka jana, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilifunga moja ya
akaunti za TFF, ambayo mdhamini wa Ligi Kuu Kampuni ya Vodacom, ilikuwa
imeingiza fedha kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo, kutokana na
limbikizo la kodi za makocha wa kigeni kuanzia enzi za Mbrazil Marcio
Maximo.
Baada ya kukwama kwa juhudi za TFF kutaka TRA irejeshe fedha hizo ili
kuokoa Ligi Kuu, Januari 5, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Amos Makalla, alikutana na pande zote zinazohusika katika
sakata hilo ambazo ni TRA, TFF na klabu, wakijadili pia utitiri wa
makato kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kilifanyika baada ya Klabu za Ligi Kuu kutaka zipatiwe
fedha hizo hadi kufikia leo, walau kuwa na siku 10 za kujiandaa kabla ya
kuanza kwa ligi hiyo, vinginevyo hawatacheza ligi hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, kuhusu hatima
ya ligi hiyo kutokana na msimamo huo wa klabu, Mkurugenzi wa Mashindano
wa TFF, Saad Kawemba, alisema raundi ya pili ya ligi hiyo itaanza siku
hiyo kama ilivyopangwa awali, akiamini muafaka utapatikana kwenye kikao
cha leo baina ya pande zote husika.
“Raundi ya pili ya Ligi Kuu itaanza kama ilivyopangwa Januari 26,
tukiamini kikao cha kesho, kati ya pande husika, kitaisha kwa kupatikana
muafaka ili kuepusha matatizo zaidi, kwani kupitia kikao chetu cha
kwanza, serikali ilituelewa vizuri, tunaamini itakuja na majibu mazuri,”
alisema.
Hoja kubwa ya TFF katika utetezi wao ni kuwa, kwa vile makocha wa
kigeni wote wamekuwa wakilipwa na serikali, TRA haikupaswa kukamata
akaunti ya shirikisho hilo, hatua ambayo inaweza kuleta matatizo makubwa
katika soka kwa klabu kushindwa kusafiri.
No comments:
Post a Comment