MAPIGANO makubwa yamezuka katika mikoa ya Morogoro na Mtwara
kiasi cha kusababisha kifo cha mtu mmoja, Mohamed Msigala (60), na
kuharibiwa kwa magari na mali nyingine ikiwemo kuchomwa moto kwa
mahakama ya mwanzo.
Mapigano yaliyozuka mkoani Morogoro yamehusisha wakulima wa vijiji vya
Msolu, Mbigili, Mambengwa na Mabwegere vilivyoko kata ya Dumila, wilaya
ya Kilosa, mkoa wa Morogoro, yakiwaacha mamia ya wanawake na watoto
wakiyakimbia makazi yao kwa hofu ya kuuawa.
Mapigano hayo yametokea kati ya wakulima na wafugaji wa vijiji hivyo
wanaogombea ardhi, inayodaiwa kuuzwa kinyemele kwa baadhi ya mawaziri
waandamizi na wafugaji, huku kukiwa na tishio la kufutwa kwa baadhi ya
vijiji.
Mali kadhaa yakiwemo magari yameharibiwa vibaya, ambapo nyumba tano za
kulala wageni katika eneo la Dumila zimeshambuliwa, wananchi kupora
mali mbalimbali zinazodaiwa kumilikiwa na wafanyabiashara wa jamii ya
Kimasai.
Mapema majira ya saa 2:30 asubuhi, mamia ya wananchi hao walifanya
maandamano kutoka mwanzo hadi mwisho wa mji huo na kutanda kwenye
barabara, kabla ya kuiziba kwa mawe na magogo makubwa na kuchoma
matairi.
Kikosi cha polisi cha kutuliza ghasia kililazimika kuingilia kati na
kupambana na waandamanaji hao kwa mabomu ya machozi na virungu na
kufanikiwa kuwakamata idadi kubwa ya wananchi hao.
Pamoja na barabara hiyo ya Morogoro – Dodoma lakini pia wananchi hao
walifunga barabara ya Dumila- Kilosa na hivyo kuyafanya magari
yaliyokuwa yakitumia barabara hiyo kusimama kwa muda mrefu.
Habari zinasema kuwa vurugu hizo zimechochewa zaidi baada ya wafugaji
wa jamii ya Kimasai kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mazao, lakini
hakuna hatua zozote zilizochukuliwa licha ya uongozi wa kijiji hadi mkoa
kufikishiwa malalamiko hayo.
Mashamba yanayolalamikiwa yako katika eneo la Mabwegere ambalo
linadaiwa kuuzwa kwa baadhi ya mawaziri, na hivi karibuni Mkuu wa Wilaya
ya Kilosa Elias Tarimo alitangaza kuwa ni mali ya wafugaji jambo ambalo
lilipingwa na wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera alilazimika kukatisha shughuli
zake za Kibunge huko Dodoma na kurejea mkoani Morogoro kuangalia hali
ilivyo.
Hata hivyo, akihojiwa kwa njia ya simu, Bendera alionekana kufura
akidai kwamba kulikuwa na upotoshaji mwingi uliochangia kutoeleweka vema
kwa suala hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile,
amethibitisha kukamatwa kwa watu kadhaa katika vurugu hizo na kwamba
ulinzi umeimarishwa.
Tuhuma za kuhusika kwa baadhi ya mawaziri katika serikali ya Rais
Jakaya Kikwete, huku mmojawao akidaiwa kununua hekari 400, zilianikwa
mapema mwezi jana, huku mamlaka zikiwa zinataka kufuta hati miliki ya
kijiji cha Mabwegere.
Ilielezwa kuwa watu wasiojulikana waliingia kijijini hapo na kuingilia
mipaka na kung’oa alama zilizowekwa na serikali licha ya kuamriwa kuwa
mahakama itekeleze zoezi hilo baada ya wanakijiji hao kushinda kesi.
Mbali na kung’olewa kwa mipaka hiyo, watu kutoka maeneo mbalimbali
waliendelea kuingia katika kijiji Mabwegere kinyume cha utaratibu na
kufungua mashamba ambayo yanadaiwa kumaliza maeneo ya malisho ya mifugo
iliyomo kijijini humo. Kijiji cha Mabwegere ni cha wafugaji ambacho
ndicho kilichoathiriwa zaidi na machafuko.
Kwa mujibu wa barua yao ya malalamiko, wananchi hao walisema kuwa kwa
sasa wamepoteza imani na mkuu wa wilaya na mkurugenzi wao kwani
walitegemea kuwa migogoro ya ardhi iliyosababishwa na wakulima
kujichukulia eneo la wafugaji ingetatuliwa kwa kuzingatia sheria na
utawala bora.
Ofisa mtendaji mstaafu wa kijiji hicho, Sadiki Mwibela, alisema kuwa
migogoro mikubwa imekuwa ikitokea kati ya wakulima na wafugaji.
“Kwa sasa msimu wa mvua umeanza, machafuko yanaweza kutokea, lakini
mimi kwa kuwa nilikuwa nafuatilia haki za wafugaji waliokuwa wanaporwa
mifugo yao kwa kuwa tulikataa kuuza eneo letu, nilifukuzwa kazi,
nikakamatwa nikapelekwa jela, nilipotoka nikakuta wameweka mtendaji
mwingine,” alisema.
Viongozi wengine ambao waliomba wasitajwe gazetini walisema kuwa
walilazimishwa na mkuu wa wilaya kwenda ofisini na kuandika muhtasari
ili waziri huyo apewe eneo.
Mtwara hakukaliki
Mkoani Mtwara wananchi wamechoma moto mahakama ya mwanzo na kuharibu gari la polisi, kufuatia kuzuka kwa mapigano kati yao jana.
Mapigano hayo yalianza baada ya askari polisi kuwavamia wananchi
katika eneo la Sabasaba waliokuwa wamefurika kushuhudia watu
wanaoaminika kuwa wachawi walionaswa usiku wakifanya vitendo vya
kishirikina.
Mmoja wa wananchi walioshuhudia tukio hilo, amesema kuwa polisi
waliokuwa ndani ya gari wakiwa na bunduki, walifika eneo hilo baada ya
kupewa taarifa na msamaria mwema kuwa kulikuwa na vurugu za wananchi
waliotaka kuwaua watu hao wawili waliokutwa wakifanya vitendo hivyo vya
kishirikina.
Hatua hiyo ya polisi, iliwakasirisha wananchi walioamua kujibu mapigo
kwa kuwashambulia kwa mawe na kisha kuharibu gari lao na kulazimika
kukimbia kusalimisha maisha yao.
Habari zinasema kuwa askari polisi walirudi wakiwa katika magari
matatu na ndipo walianza kuwashambulia wananchi popote walipowakuta
katika eneo la soko kuu la Mtwara na kuharibu mali.
Wananchi nao waliamua kujikusanya kwa wingi na ndipo yakazuka
mapambano mengine makubwa yaliyosababisha kuchomwa moto kwa mahakama
hiyo.
Kamanda wa polisi wa mkoa hakuweza kupatikana, kwa vile simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani kwa muda mrefu.
Polisi waonya
Jeshi la polisi nchini, limewataka wananchi kutii sheria bila
shuruti, na wasitumie mwanya wa makosa yanayofanywa na baadhi ya askari
au wananchi wengine waliovunja sheria kuhalalisha uvunjaji mwingine wa
sheria, kwani makosa mawili hayafanyi haki moja.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, aliiambia Tanzania Daima
Jumamosi kuwa ni jambo baya na la hatari ikiwa sasa wananchi wataamua
kuchukua sheria mikononi kuvamia vituo vya polisi na kuua askari, au
kuvamia mali za watu.
Senzo amelalamikia vitendo vinavyozidi kushamiri nchini kwa wananchi
kuvamia vituo vya polisi, kuchoma moto vituo, au wananchi kuacha kabisa
kutii amri halali za jeshi la polisi pindi askari wanapofika katika
maeneo yenye fujo.
Alikiri kuwa ndani ya jeshi hilo kuna askari wachache wakorofi ambao
sio waadilifu, lakini huo sio mwanya kwa wananchi kuhalalisha, kujeruhi
au kuvamia vituo vya polisi.
“Tunakataza uvunjaji wa sheria iwe ni kwa askari au raia, ndio maana
inapothibitika kuwa polisi amekosea, anachukuliwa hatua kwa mujibu wa
sheria za jeshi,” alisema.
Makachero wavamia vyuo
Katika hatua nyingine watu wanaoaminika kuwa makachero wa serikali,
wameingia mkoani Mtwara na sasa inadaiwa wanaendesha uchunguzi wa siri
wenye lengo la kuwabaini watu wanaotuhumiwa kuwa vinara wa kupinga
ujenzi wa bomba la gesi.
Habari za kuaminika zimesema kuwa makachero hao walianza kuwasili
mjini hapa, siku sita zilizopita na wamejizatiti katika baadhi ya
taasisi nyeti vikiwemo vyuo vya elimu ya juu, kunakoaminika kuwa moto wa
hamasa wa kupinga ujenzi huo umeshika kasi.
Mbali na vyuoni, makachero hao wamekuwa wakiendesha uchunguzi katika
ofisi za serikali, kujua ni wafanyakazi gani wanaoshabikia jambo hilo na
kwamba watakaobainika watakamatwa na kufunguliwa mashtaka mbalimbali
yakiwemo ya uchochez
Habari na na Ghisa Abby na Josephat Isango
No comments:
Post a Comment