MPANGO mchafu wa kukichafua Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) mkoani Iringa umefichuka, huku Makamu Mwenyekiti wa CCM bara,
Philipo Mangula akituhumiwa kuratibu harakati hizo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya CCM, zimebainisha kuwa, chama
hicho kimechapisha mamia ya kadi za CHADEMA ambazo zimesambazwa kwa watu
maalumu walioandaliwa ambao wameambiwa wazirejeshe leo wakati wa
mkutano wa hadhara na kumkabidhi Mangula, wakidai wameihama CHADEMA.
Imebainika kuwa, zaidi ya wanafunzi 200 wa Chuo Kikuu kishiriki cha
Mkwawa tayari wamekabidhiwa kadi hizo, na fedha za kujikimu ambapo
watajitangaza kama wana-CHADEMA waliohamia CCM baada ya kuchoshwa na
upinzani katika viwanja vya Mwembetogwa Manispaa ya Iringa.
Mbali na kadi, CCM pia imetengeza fulana za CHADEMA walizopewa
wanafunzi hao, na kwamba chama hicho kimemwaga maelfu ya fedha kwa
wasomi hao kama njia ya kufanikisha mpango huo.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, Mtama Joseph
amekiri kusikia taarifa hizo, lakini akadai kuwa kama ni kweli basi,
utakuwa ni mpango unaotumika na watu waliopoteza mwelekeo.
“Ni kweli kuna taarifa hizo zimezagaa hapa chuoni kwamba kuna
wanafunzi 200 ambao wamepewa sh 5,000 kila mmoja, na kadi zenye nembo ya
CHADEMA ili warudishe kwenye mkutano wa CCM utakaofanyika kesho (leo)
katika viwanja vya Mwembetogwa,” alisema.
Mtama alisema kama habari hizo ni za kweli, litakuwa jambo la
kusikitisha na linaloonesha kuwa watu walioshindwa kufikiri na
kuwajibika hutumia mbinu chafu kwa kuwa hawana fikra zingine zaidi ya
rushwa.
Mmoja wa vijana wanaodaiwa kutumiwa katika mpango huo (jina
limehifadhiwa) amekiri kuwa miongoni mwa viongozi wanaoratibu mpango huo
na kwamba yeye na wenzake wameahidiwa sh 500,000 kila mtu pindi
watakapofanikisha hujuma hiyo.
Kijana huyo aliyeomba jina lake lisitajwe kwa kuhofia usalama wake,
alisema tayari kuna vijana 17 ambao wameandaliwa pamoja na kuratibu,
lakini pia kufanya kazi ya kuichafua CHADEMA kwa namna watakavyoelekezwa
pindi wakifika mkoani hapa kwa ajili ya mikutano ama shughuli nyingine.
Mbali na hilo, kijana huyo alisema CCM pia imeandaa magari kusomba
wanachama wake kutoka vijijini kuletwa katika mkutano wa leo kwa madai
ya kutaka ionekane ina wanachama wengi, hivyo kuondokana na aibu ya
kukosa watu katika mkutano wake.
Katibu wa CHADEMA Manispaa ya Iringa, Suzan Mgonukulima alisema kuna
mbinu chafu zilizobainika kutumika kuhujumu CHADEMA ambazo wananchi
wanatakiwa kuwa nazo makini.
Alisema kufichuka kwa siri hizo, ni ishara wazi kuwa watu
wanaojitangaza kurudi CCM sio wanachama halisi, bali waigizaji na kuonya
kuwa mchezo huo ni ishara ya wazi kuwa sasa serikali inatishiwa na
CHADEMA.
Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi (CHADEMA) ambaye pia ni
mjumbe wa kamati tendaji ya wilaya, alisema propaganda za CCM zimepitwa
na wakati na kwamba ni dalili za kutapatapa kwa sababu wanajua kuwa
mwaka 2015 wanaachia ngazi.
Wabunge CHADEMA waishukia serikali
Jijini Dar es Salaam, wabunge wawili wa CHADEMA, Mchungaji Peter
Msigwa (Iringa Mjini) na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini)
wameufananisha uongozi wa Serikali ya CCM na ule wa kifalme uliofitinika
kutokana na mawaziri wake kutofautiana katika maamuzi mbalimbali ya
kitaifa.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi Mombasa jijini
Dar es Salaam, wabunge hao walisema mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya
Kikwete, hawaelewani hali inayoweza kuifanya nchi kuwa katika hatari ya
kushindwa kufanya mambo ya maendeleo kwa wakati.
Mchungaji Msigwa, alisema hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Uratibu na Mahusiano), Stephen Wasira aliwaamuru wananchi waendelee
kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
wakati akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Alisema katika hifadhi ya Serengeti kuna mlango unaotumiwa na wanyama
na kwamba Wasira akijua sheria hairuhusu kufanya shughuli za kibinadamu
katika eneo lolote la uhifadhi aliwahimiza wananchi wajenge nyumba na
shughuli za kilimo hadi alipoonywa na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki.
“Wanasema CHADEMA itakufa wakati wao ndio wanaelekea kuzimu kama huyu
Wasira aliyeonywa na Kagasheki juu ya kuhamasisha uvunjifu wa amani
katika eneo hilo la Serengeti, lakini ameendelea kupuuza na kusema ni
heri afe kuliko kufuata taratibu,” alisema Msigwa.
Akizungumzia ujangili katika mkutano huo, Msigwa alisema serikali
inapaswa kupanga mipango madhubuti kukabiliana na hali hiyo badala ya
mawaziri wake kutumia muda mwingi kutaka kuihujumu CHADEMA.
Alisema kutokana na udhaifu huo wa Baraza la Mawaziri na hofu ya
kuondolewa madarakani ifikapo 2015, wameshindwa kuunganisha nguvu ya
pamoja za idara ya ulinzi na usalama hata kufikia baadhi ya watendaji
kujiingiza katika matukio ya ujangili kama ilivyotokea hivi karibuni kwa
askari wa Jeshi la Wananchi kukutwa akisafirisha pembe za ndovu.
Kwa upande wake, Sugu aliitaka serikali iache kuwahadaa wananchi kwa
kutumia nguvu kubwa kuonesha mafanikio ya serikali katika vituo vya
runinga wakati wananchi wana hali ngumu ya kimaisha.
“Kama utaangalia mafanikio ya nchi yetu kwenye runinga unaweza kusema
tumepiga hatua kubwa katika kilimo, lakini niwaambieni hali ni mbaya kwa
wakulima na nilifikiri serikali inaweza kuwa ya kiungwana na kuelezea
matatizo halisi yanayowakabili,” alisema Sugu.
Aliongeza kuwa serikali imetumia gharama kubwa kuelezea mafanikio
yasiyokuwepo, na haijulikani fedha zinazotumika kulipia matangazo hayo
zinatoka katika mfuko gani.
Sugu alisema hali ilivyo sasa ni wazi CCM wanaomba Mungu 2015 isifike
kwa kuwa wanajua mwaka huo ndiyo mwisho wa safari ya muda mrefu
waliotumia kuwanyima maendeleo Watanzania.
No comments:
Post a Comment