Marehemu Omari Omari atazikwa January 9 2013 |
MWANAMUZIKI mahiri wa miondoko ya Mchiriku, Omari Omari (41),
aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana na anatarajiwa kuzikwa leo saa 7
mchana katika makaburi ya Maganga, Temeke Mikoroshini jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza nyumbani kwao Temeke Mikoroshini jana, dada wa marehemu,
Vingawaje
Omari alisema, mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa leo saa 6
mchana, kabla ya mazishi baada ya kukamilika kwa taratibu zote, ikiwa ni
pamoja na kuwasili kwa ndugu na jamaa kutoka sehemu mbalimbali.
Vingawaje alisema, marehemu alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya kifua.
Januari 5 alizidiwa na kukimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Temeke
na juzi aliruhusiwa kabla ya kukutwa na umauti nyumbani kwao Temeke
Mikoroshini, saa 8 usiku wa kuamkia jana.
“Nimepokea msiba huu kwa masikitiko makubwa, ukizingatia kwamba mimi
ndiyo mkubwa wa marehemu katika familia ya watoto saba, hivyo ni pigo
kwangu na familia kwa ujumla, kwa kuwa tumempoteza ndugu yetu
tuliyemtegemea,” alisema Vingawaje.
Katiha enzi ya uhai wake, Omari aliwahi kutamba katika tasnia hiyo
kupitia wimbo wake wa
‘Kupata Majaliwa’ ulibeba albamu na kurekodiwa
katika studio ya Dhahabu Tabata, jijini Dar es Salaam, akishirikiana na
kikundi cha Atomic.
Mmoja wa wasanii aliyeshirikiana na marehemu katika kundi hilo ni
Mfaume Suleiman ‘Dogo Mfaume’, aliyesema amepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa za msiba huo.
“Nimesikitishwa sana na taarifa za msiba, kwani nimempoteza ndugu
yangu niliyemtegemea kwa kiasi kikubwa, kwani amenisaidia kwa kiasi
kikubwa kujulikana katika tasnia ya muziki, kwa kuwa yeye ndiye
aliyenitungia nyimbo ya ‘Kazi ya Dukani’ wimbo ambao bila yeye
nisingeufanya,” alisema Dogo Mfaume.
Naye mwandaaji wa muziki kutoka katika studio ya Mkubwa na Wanawe,
Promota Bonga, alisema kuwa, amesikitishwa na kufariki kwa mwanamuziki
aliyetarajia kumshirikisha katika kazi mbalimbali za muziki, kutokana na
uwezo aliyokuwanao wa kupiga vyombo vya muziki na kuimba.
“Tumempoteza mtu muhimu mno katika tasnia ya muziki, kwani amewainua
chipukizi wengi, kwa kuwa alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga kinanda
pamoja na ngoma, hivyo tunashukuru kwa kuwa ni mipango ya Mungu,”
alisema Bonga.
No comments:
Post a Comment