KINA mama wajawazito ambao wamewekwa katika nyumba ya
kujitazamia kwa ajili ya kusubiri kujifungua maarufu kwa jina la
(Chikande) katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wamelalamikia huduma mbovu
zinazotolewa katika nyumba hiyo ikiwa ni pamoja na kukuthiri kwa
kunguni.
Malalamiko hayo yalitolewa na baadhi ya akina mama wajawazito
walipokuwa wakizungumza na Tanzania daima iliyotembelea eneo hilo kwa
ajili ya kujionea hali akina mama hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kina mama hao walisema katika nyumba
hiyo kwa sasa wanaishi katika mazingira magumu kutokana na kutopata
huduma ambayo inastahili.
Mbali na hilo walisema idadi ya wagonjwa wanaopokelewa katika nyumba
hiyo kwa sasa imezidi na kuwafanya wagonjwa wengine kulala chini huku
wengine wakilala wawili hadi watatu katika kitanda kimoja.“Kituo hiki kina uwezo wa kupokea wagonjwa 30 kwani kuna vitanda 15
ambapo kila kitanda tunalala watu wawili lakini kwa sasa idadi imezidi
hadi kufikia wagonjwa 100 hali inayosababisha kuwepo kwa msongamano
mkubwa kutokana na uhaba wa vitanda hivyo wagonjwa wanalazimika kulala
watatu katika kitanda kimoja na wengine kulala chini…
“Licha ya wagonjwa kulala chini lakini bado wagonjwa wengine
wanalazimika kupokezana kwa wengine kulala nje kwani hawawezi kutosha
kulala nyumba moja wote kwa wakati mmoja jambo ambalo walidai kuwa ni
hatari kwa afya zao,” alisema mmoja wa kina mama hao aliyejitabulisha
kwa jina la Mwalu Mboje .
Aidha mgonjwa mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Monica Silla (29)
aliyetokea Kijiji cha Ng’hambabu Wilaya ya Chamwino, mkoani hapa
amesema kituo hicho kinakabiliwa na tatizo la kunguni na mbu, hali
inayohataraisha afya zao.
Monica aliweka wazi kuwa tayari walisha wasilisha malalamiko yao kwa
wauguzi kituoni hapo lakini hakuna jitihada zilizofanywa wala bwana afya
yeyote aliyewahi kutembelea kituoni hapo ili kujua changamoto
wanazokumbana nazo.
Nyumba hiyo ya Chikande iliyopo ndani ya hospitali ya Mkoa wa Dodoma
inapokea kina mama wajawazito kutoka wilaya za Bahi, Chamwino, Manyoni
na vijiji vya pembeni katika Wilaya ya Dodoma Mjini wenye matatizo
wakati wa kujifungua, ikiwa na wale ambao ni walemavu, wenye ugonjwa wa
kifafa na wale waishio mbali na vituo vya huduma za afya.
Kutokana na matatizo yanayoikabili nyumba hiyo, alipotafutwa kwa njia
ya simu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya,
simu yake iliita bila majibu na baada ya dakika 5 simu yake iliita na
kupokewa na baada ya mwandishi kujitambulisha tu alikata simu. HABARI NA MARTIN MALERA WA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment