Baadhi ya wanakijiji wakiangalia masalia ya gari lililoteketezwa moto lenye namba za usajili T 654 BNB aina ya Gumsam linalodaiwa kuwa ni mali ya mmoja kati ya polisi wawili waliouawa Jumapili usiku (Januari 6, 2013) katika kitongoji cha Kituntu, Kijiji cha Kasheshe, Kata ya Rugu wilayani Karagwe mkoani Kagera.
ASKARI wawili wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira na gari lao kuchomwa moto wakituhumiwa kuwa ni majambazi.
Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kasheshemisha, Kata ya Rugu Wilaya hiyo Jumapili iliyopita, mishale ya saa 2:30 usiku.
Akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Karagwe chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Darry Ibrahim Rwegasira na ya Mkoa iliyoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Phillipo Kalangi na viongozi wengine wa serikali wilayani humo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasheshemisha, Sadick Mohamed, alisema walipata taarifa kutoka Kijiji cha Rugu kuwa kuna majambazi walifika majira ya saa 12:00 jioni na wakati wakijaribu kuondoka, wanakijiji waliweka kizuizi barabarani na kuwaamuru wasimame.
Mohamed alisema watu hao hawakutii amri na kupita kwa nguvu katika eneo hilo ndipo walipoamua kupiga simu kwa mwenyekiti huyo ambaye naye alitoa taarifa kwa wananchi wake na kuziba barabara kwa mawe.
Alisema gari lao lilipofika Kijiji cha Kasheshemisha, lilikuta mawe barabarani na kushindwa kupita ndipo wananchi waliwaamuru wajisalimishe, lakini walikaidi na kuanza kufyatua risari hewani huku wakitafuta njia ya kuwawezesha kutoroka.
Alisema walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili na kutokana na hasira ya kurushiwa risasi, waliwapiga hadi kuwaua kisha walipopekua ndani ya gari walikuta meno saba ya tembo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, hasira za wananchi zilipanda zaidi walipogundua mwenzao amejeruhiwa na risasi na kuamua kuyatoa meno hayo ya tembo saba na kulitekeleza gari hilo lenye namba za usajili T 654 BNB.
Mohamed alisema mwanakijiji huyo, Jovinary Joseph aliyejeruhiwa na risasi kwenye kiganja, alikimbizwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga kwa matibabu.
KAULI YA KAMANDA
Kamanda Kalangi aliwashukuru wakazi wa Kijiji cha Kasheshemisha kwa ushirikiano waliounyesha katika kukabiliana na watuhumiwa hao.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwaeleza kuwa kila raia ana haki ya kuishi kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo aliwaasa na kusema si vema kujichukulia sheria mkononi kama walivyofanya.
Alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanyika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
DC AZUNGUMZA
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Darny Ibrahimu Rwegasira, aliwapongeza wakazi wa Kijiji cha Kasheshemisha na kuwataka kuimarisha zaidi kamati za ulinzi na usalama katika ngazi za kata, vijiji, vitongoji na mitaa.
Aidha, aliwaasa kutii amri halali mahali popote inapotolewa na kusema kuwa iwapo watuhumiwa hao wangetii amri walipotakiwa kusimama, huenda wasingefikwa na mauti hayo.
Askari waliokufa wametambuliwa kwa majina ya Sajenti Thomas Migiro na Koplo Damas Kashala kutoka Benako wilayani Ngara.
Askari mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Braiton, anadaiwa kujisalimisha katika kituo kidogo cha polisi.
MGANGA HOSPITALI YA WILAYA
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Andrew Cesari, amethibitisha kupokea miili ya marehemu wawili ambao majina yao hayakutambulika na kwamba uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa chanzo cha mauti hayo ni majeraha.
Desemba 15, mwaka jana katika Kijiji cha Mugoma wilayani Ngara, polisi wawili waliuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kufanya mauaji ya raia, Said Mkonikoni, hali iliyosababisha hasara kubwa ikiwa ni pamoja na kuteketezwa kwa moto kituo kidogo cha Polisi cha Mugoma.
Baadhi ya polisi wa mkoa wa Kagera wameripotiwa kukamatwa juzi wilayani Serengeti mkoa wa Mara wakisafirisha meno ya tembo kinyume cha sheria.
Jeshi hilo limedai linaendelea na uchunguzi na kwamba itakapothibitika wahusika watafikishwa mahakamani wakati wowote.
No comments:
Post a Comment