SAKATA la mtuhumiwa, Joshua Mulundi, anayekabiliwa na kesi ya
kumteka na kutaka kumsababishia kifo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
nchini, Dk. Steven Ulimboka, sasa limechukua sura mpya baada ya kudaiwa
kuondolewa kiaina katika mahabusu ya Gereza la Keko na kufichwa katika
selo ya adhabu.
Chanzo chetu ndani ya mahabusu hiyo kilieleza kuwa mshitakiwa huyo
ambaye ni raia wa Kenya, alikuwa ameanza mgomo wa kutokula, kisha
kupanda juu ya paa la gereza hilo, akitishia kujiua endapo wapelelezi wa
kesi yake hawatafanya juhudi za kumleta Dk. Ulimboka ili amtambue.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mulundi baada ya kukaa juu ya paa na
kunyeshewa mvua kwa saa kadhaa akiwa na mahabusu wenzake, uongozi wa
gereza ulitumia nguvu za ziada kuwashusha watuhumiwa hao kwa nguvu huku
mtuhumiwa huyo akipatiwa kipigo kikali kabla ya kuhamishwa.
Kwamba, Magereza waliwaleta baadhi ya askari wake wa Kikosi Maalumu
cha Kuzuia Fujo, ambao inasemekana walimcharaza Mulundi na wenzake na
kisha kumwondoa ndani ya mahabusi hiyo na kupelekwa sehemu
isiyojulikana.
Tanzania Daima ilifanya juhuzi za kuzungumza na msemaji wa Magereza,
Omary Mtiga, lakini hakuwa na ushirikiano wa kutosha, badala yake alitoa
maneno ya kejeli kwa gazeti hili kuwa linaandika habari za kizushi.
“Mimi ndiye msemaji wa Magereza, huo umbea unaopenyezewa na hao
wanaojiita vyanzo vya ndani, si ‘official’ (rasmi). Mulundi anachotaka
ni kuonana na hakimu kwa tarehe aliyopangiwa,” alisema.
Mtiga bila hakukubali wala kukataa, alipoulizwa uongozi wa gereza hilo
umemsaidiaje kufikia anachokitaka kama mahabusu mwenye haki zake,
alijibu kwa hasira kuwa hayo ni mambo ya ndani ya utawala.
“Wewe kama unataka kufanya uchunguzi wa kina wa jambo hili
unalolihangaikia, njoo ufungwe gerezani, utapata yote. Hayo unayoniuliza
ili niseme amepelekwa wapi ni mambo ya ndani, hayawahusu kuandika,”
alisema.
Mtiga ambaye alikuwa akizungumza kwa mkato kwenye simu yake ya
kiganjani, alihoji kama mwandishi anaweza kuandika masuala ya mgogoro wa
ndoa yake hadharani na kusisitiza kuwa; ‘Hayo mambo ya kutafuta habari
za hovyo hovyo yaacheni.”
Alisema kuwa anashangazwa kuona Tanzania Daima lilivyolivalia njuga
sakata hilo wakati mshitakiwa Mulundi ni mahabusu kama wengine, asiye na
sifa yoyote ya pekee.
Mtiga licha ya kusisitiza kuwa mahabusu huyo hajagoma kula, bado
hakuweza kuthibitisha amehamishiwa gereza gani, akisema hiyo ni siri ya
utawala.
Gazeti dada na hili la Tanzania Daima Jumapili iliyopita lililitoboa
siri jinsi Mulundi anavyoitaka serikali imlete mbele yake Dk. Ulimboka
ili afanyiwe gwaride la utambulisho kubaini kama alihusika katika tukio
la kumteka.
Imeelezwa kuwa amechukua uamuzi huo mgumu baada ya kutoridhishwa na
mwenendo wa kesi ambayo tangu Julai 3, mwaka jana bado iko kwenye hatua
ya upelelezi na hajui utakamilika lini.
Askari mmoja wa Jeshi la Magereza kutoka ndani ya gereza hilo alikiri
kuwa mtuhumiwa huyo amegoma na usiku wa kuamkia juzi alishinda juu ya
paa la gereza hilo akinyeshewa mvua.
Habari zaidi zinasema kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambaye hana wakili
mahakamani, wamewasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kutoa msaada wa
kisheria.
Kwa mujibu wa ndugu hao, hadi sasa hawaoni maendeleo ya kesi hiyo
kwani kila ikifika mahakamani upande wa mashitaka hutoa hoja ya kutaka
iahirishwe kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.
Hata hivyo Mulundi anadai kuwa amewahi kutoa malalamiko kwa Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Angela Kairuki na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiiomba serikali
imlete mbele yake Dk. Ulimboka ili amtambue na kuhakikisha upelelezi wa
kesi hiyo unafikia tamati.
Dk. Ulimboka ambaye alikuwa kinara wa mgomo wa madaktari uliotikisa
nchini kwa wakati tofauti mwaka jana; alitekwa, kuteswa, kupigwa hadi
kung’olewa meno na kucha na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, alitangaza kuunda tume ya wataalamu kutoka ndani ya
jeshi hilo iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja baadhi ya
watu aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini hadi sasa
Mulundi ndiye mtuhumiwa pekee aliyekamatwa.
Hata hivyo tume hiyo haijawahi kutoa ripoti yake kama Kova alivyoahidi
pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka hajahojiwa, huku
vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana na sakata hilo.
Hivi karibuni jeshi hilo kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso,
limekanusha kuwapo kwa tume hiyo, likisema walioteuliwa ni polisi ambao
watafanya kazi za kiuchunguzi kwa taratibu za polisi.
Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye hivi karibuni alikiri
kuwapo kwa tume hiyo, lakini akasema hawezi kulizungumzia suala hilo
kwa vile taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu baada
ya kukamilisha wajibu wake.
Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk.
Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo
yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi.
CHANZO CHA HABARI NI TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment