SERIKALI imepiga marufuku tabia ya baadhi ya walimu kuwarudisha
wanafunzi nyumbani kwa sababu ya kutolipia michango mbali mbali ya
shule na kwa kukosa sare za masomo.
Hayo yalibainishwa juzi na Naibu Waziri kutoka ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa, Mhe Aggrey Mwanri alipokuwa
akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika uwanja wa Kashaulili mjini Mpanda akihitimisha ziara yake
katika halmashauri ya mji wa Mpanda.
Naibu Waziri TAMISEMI, Aggrey Mwanri akimuweka kitimoto Mganga
Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda, Dr Kamgobe baada ya
kulalamikiwa na akinamama kuwa wanatozwa pesa pindi wanapokwenda
kujifungulia katika vituo vya huduma za afya vya serikali hasa
zahanati katika mikutano ya hadhara wilayani humo, katikati mwenye
suti ya bluu ni mkuu wa wilaya hiyo Paza Mwamlima.
|
Na Willy Sumia, Mpanda
Alisema kumekuwa na mtindo kwa baadhi ya shule kuwarudisha wanafunzi
nyumbani kwa kisingizio cha kukusanya michango lakini wanasahau kuwa
muda ule ni muda wa masomo kwani siku na saa za masomo zimehesabiwa na
inapopotea dakika moja kwa mwanafunzi kukaa bila kusoma haiwezi
kufidiwa tena hivyo serikali imeliona na kuamua kuchukua hatua.
Alisema kuanzia jana (Januari 20,2013) hakuna kumrudisha mwanafunzi wa
shule ya msingi na sekondari kwa sababu hajamalizia michango ya shule
na wala eti kwa sababu hana sare za shule husika, badala yake walimu
washirikiane na uongozi wa kata kuwawajibisha wazazi wasiokamilisha
michango shuleni na kuwanunulia wanafunzi sare za masomo.
'' Walimu nisikilizeni, kuanzia leo hakuna ruhusa kwa mwalimu
kumrudisha mwanafunzi nyumbani eti kutafuta michango, mnataka
wakafanye vibarua huko? Mzigo wa michango ya shule na sare ni wa
wazazi na walezi wao siyo wa mtoto tena msiwape barua watoto
kuwapelekea wazazi wao, pelekeni katika ofisi za kata kuna kamati ya
maendeleo ya Kata WDC" alisema Mhe. Mwanri
Alisema unapomrudisha mwanafunzi nyumbani akachukue mchango wa shule
maana yake ni kwamba asirudi shule kama hajapewa mchango na hapo ndipo
unadhoofisha maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma hivyo kama umeajiriwa
na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huruhusiwi kuwarudisha
wanafunzi wakatafute michango
Akizungumzia michango mingi mashuleni Mwanri alisema hivi sasa
serikali imebadili utaratibu wa kurasimisha michango kwa kupitia ofisi
ya Katibu Tawala wa Mkoa husika na hivyo kila shule itakayokaa na
wazazi na kupanga michango yao ya shule kwa maendeleo ya shule yao
lazima kwanza mapendekezo hayo yapelekwe kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo
ili ayapitie mapendekezo hayo na kujiridhisha ndipo atoe kibali cha
kuanza kutoza michango hiyo
Alisema hivi sasa kila shule ianze utaratibu wa kuita wazazi na
kuangalia ichakavu wa madawati yaliyopo na kutolea mapendekezo ya
ukarabati wake ili yaweze kutumika badala ya kuendelea na mtindo wa
kila mwaka wanafunzi kudaiwa kwenda na madawati shuleni kwani kila mtu
anajiuliza madawati hayo hayajai shuleni huko, ni bora uwepo utaratibu
wa kuangalia mapungufu ndiyo yachangiwe na wazazi
Aliwaagiza wakurugenzi watendaji katika halmashauri kukagua na
kujiridhisha namna majembe, mapanga na madawati yanavyotumika
mashuleni kwani kuna baadhi ya sehemu wanafunzi wanaagizwa kuwenda na
majembe mapya yenye mpini lakini wakifika shuleni majembe mapya
yanakusanywa na kuwekwa badala yake siku ya kulima ikifika wanafunzi
wanagawiwa majembe ya zamani.
Naibu Waziri Mwanri anatarajia kukamilisha ziara yake katika mkoa wa
Katavi Jumatano na kurejea mjini Dodoma kwa ajili ya kikao kijacho cha
bunge.
No comments:
Post a Comment