BAADHI ya viongozi wa dini nchini wamemtaka Katibu wa Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye, kufuta kauli yake ya kuhusisha kanisa na masuala
ya ufisadi yanayotokea nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Maadili na Haki za Binadamu kwa Jamii, Mchungaji William Mwamalanga,
alisema kuwa kauli iliyotolewa na kiongozi huyo dhidi ya kanisa ni ya
uchonganishi kwa jamii.
Mwamalanga alisema kuwa kutokana na kauli hiyo wamemtaka kiongozi huyo
kuliomba radhi kanisa ndani ya saa 48 kwa kitendo hicho cha kulihusisha
kanisa la ufisadi.
“Hawezi kusema kuwa kanisa la hapa nchini ndilo linachangia Watanzania
kukosa dawa katika hospitali zetu kwa madai kuwa tumekuwa tukipokea
watu wanaohusishwa na ufisadi,” alisema.
Alisema kuwa iwapo Nape atagoma kufuta kauli hiyo basi suala hilo watamuachia Mungu kwa kuwa kisasi ni juu yake.
Mwamalanga alisema kuwa shutuma alizotoa kiongozi huyo zingekuwa na
maana iwapo angekuwa nje ya chama hicho ambacho kimekuwa mstari wa mbele
kupigania suala hilo lakini limeshindwa kufanikiwa.
“Huyu tunajua alikuwa akimlenga nani katika kipindi hicho cha Meza ya
Busara kilichorushwa na redio moja ya jijini, kama Nape anamuona
kiongozi huyo ni fisadi basi atoke ndani ya chama hicho lakini si
kuendelea kuweka uchonganishi dhidi ya kanisa,” alisema.
Mwamalanga ambaye anaongoza kamati hiyo ambayo ina viongozi wa
madhehebu zaidi ya 215, alisema kuwa kanisa halitambagua mtu kwa kuwa
limekuwa ni kimbilio la watu wote.
No comments:
Post a Comment