MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Bara, Simba, jana walirejea
nchini wakitokea Oman walikokuwa wamepiga kambi kujiandaa na raundi ya
pili ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakiwa na matumaini
kibao ya kufanya vizuri.
Kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Jumamosi, Simba itaanza kuonesha makali
yake leo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, itakapokwaana na
Black Leopards ya Afrika Kusini katika mechi ya kirafiki ya kimataifa.
Akizungumza baada ya kuwasili, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig,
alisema kambi hiyo imekuwa ya mafanikio kwa vijana wake kwani ametimiza
malengo yake kwa kiasi kikubwa.
Alisema mbali ya wachezaji kupata muda wa kukaa pamoja, kitu ambacho
ni muhimu katika kujenga mshikamano miongoni mwao, pia wamejifunza mengi
ambayo yatawasaidia kucheza kwa uelewano dimbani.
Black Leopards ya Afrika Kusini
Alisema mbali ya kuongeza mshikamano baina ya wachezaji, pia hali ya
hewa na mazingira mazuri ya huko yaliwawezesha kufanya maandalizi yao
ipasavyo, hivyo timu kuimarika zaidi kadiri siku zilivyosonga mbele.
Akizungumzia ushiriki wa Ligi Kuu inayoanza keshokutwa, Liewig alisema
ni matumaini yake kuwa kikosi chake kitafanya vizuri, hivyo kutetea
ubingwa wake ilioutwaa Mei 6, mwaka jana.
Naye nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja, alisema kambi hiyo imewafanya
kuwa kitu kimoja zaidi, hivyo kikubwa ni kucheza kwa ushirikiano
kutimizia malengo ambayo si mengine bali kushinda.
Katika hali isiyo ya kawaida, kiungo wa timu hiyo, Haruna Moshi
‘Boban’ ameendeleza vituko vyake kwani baada ya kushuka kwenye ndege,
aliwakimbia waandishi wa habari akipitia upande wa kulia mwa lango la
kutokea uwanjani hapo na kutokomea eneo la kuegesha magari.
Naye Mrisho Ngassa, alikwenda upande huo wa Boban, lakini yeye alirudi
kusalimiana pia kupiga picha ya pamoja na viongozi wa klabu hiyo chini
ya Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na wadau wengine.
Wakiwa Oman walikokwenda wakitokea Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi,
Simba ilicheza mechi tatu za kirafiki wakishinda moja na kufungwa
mbili, itaanza kampeni yake ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Bara
keshokutwa dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Simba iliyomaliza raundi ya kwanza ikiwa ya tatu nyuma ya Yanga na
Azam, imekamia kusawazisha makosa ili kutetea taji hilo ililotwaa mara
18 tangu mwaka 1965, huku mtani wake Yanga akilibeba mara 24.
No comments:
Post a Comment