MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameifunga Shule ya
Sekondari Korona iliyopo Kata ya Engutoto jijini hapa, ambayo
ilizinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mwaka 2011.
Lema alifikia uamuzi huo katika kikao cha pamoja cha mashauriano
shuleni hapo na Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Eusebi Maeda, kilichohudhuriwa
pia na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji ambaye ni Ofisa Utumishi, Eliphas
Mollel na Ofisa Elimu Sekondari, Violet Muwowoza.
Alisema kuwa aliifunga shule hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo
mengi yaliyosababisha wanafunzi kushindwa kusoma tangu ifunguliwe
Januari 14, mwaka huu.
Matatizo hayo ni pamoja na umbali unaosababisha wanafunzi na walimu
kutembea kilometa 6.5 hadi kufika shuleni hapo, hivyo kuwa na muda mfupi wa masomo.
Shule hiyo pia haina huduma ya maji safi baada ya bomba lililokuwepo
kukatwa na mamlaka ya maji kutokana na deni la sh 340,000. Pia, pamoja
na walimu watano waliopo, mkuu wa shule na msaidizi wake hawaonekani.
Kati ya wanafunzi 1,200 wa kidato cha kwanza hadi cha tatu wa shule hiyo ni wanafunzi 118 pekee ndio wanaohudhuria masomo.
Lema aliwaagiza wanafunzi hao wafike ofisini kwake na wazazi wao
kesho, huku akimtaka Diwani wa kata hiyo, Anthony Male, kwa kushirikiana
na ofisa Elimu kuwahamishia kwa mafungu wanafunzi hao katika shule
nyingine zilizomo ndani ya Jiji la Arusha.
Mbunge huyo aliahidi kutoa pampu ya kuvutia maji, vifaa vya kuzalisha
umeme wa jua pamoja na matofali 3,000 na kwamba atashirikiana na mkuu wa
wilaya na mkoa kuhakikisha shule hiyo inaboreshwa ndani ya miezi mitatu
ili kutoa fursa ya kuchukua wanafunzi wa bweni.
Naye Ofisa Elimu Sekondari, Violet Muwowoza, alijitetea kuwa yeye
angeomba kwanza afuate taratibu za kuandika barua kwa Ofisa Elimu
Kiongozi ambaye ana mamlaka ya kufunga shule, jambo ambalo Lema alisema
aendelee na taratibu zake wakati wanafunzi hao wakiendelea na masomo
katika shule nyingine.
Aidha katika utetezi wake juu ya changamoto za shule hiyo, Ofisa Elimu
huyo alisema alikwisha kuwahi kupeleka mapendekezo katika vikao vya
baraza la jiji vya kununua magari ya wanafunzi lakini yakapingwa na
kusema hata hivyo wengi wa wanafunzi waliopelekwa katika shule hiyo
wanatoka shule za mchepuo wa Kiingereza, ndiyo maana hawaripoti shuleni
hapo.
Kaimu Mkurugenzi alimuomba Lema asubiri kiitishwe kikao cha dharura
cha baraza la madiwani wa jiji, alichodai huenda kitatoka na suluhisho
zuri zaidi kuhusiana na shule hiyo.
No comments:
Post a Comment