Maafisa watatu waandamizi wa
polisi nchini Kenya, wamesimamishwa kazi kuhusiana na sakata ya mtu
mmoja ambaye aliwalaghai watu kuwa yeye ni naibu kamishna mkuu wa polisi
kwa zaidi ya miaka mitano.
Mkuu wa polisi mkoani Rift Valley John M'mbijiwe
anayedaiwa kuwa na uhusiano na mtu huyo mlaghai,John Waiganjo ingawa
alikana kumfahamu ni mmoja wa wale waliofutwa kazi.
Mwenyekiti wa tume ya kuwaajiri
maafisa wa polisi KPSC Johnstone Kavulundi, amesema maafisa hao watatu
wametajwa kuhusika kwa njia moja au nyingine na kashfa hiyo.
Wiki iliyopita, Joshua Waiganjo, alifikishwa mahakamani, kwa kujifanya afisa mwandamizi wa polisi katika mkoa wa Rift Valley.
Mshukiwa huyo amekanusha madai hayo.
Ripoti zinasema kuwa ulaghai huo ulifichuliwa,
wakati aliposafiri kwa ndege ya polisi, kwenda kuchunguza mauaji wa
maafisa 42 wa polisi waliouawa na wezi wa ng'ombe katika bonde la
Suguta, tukio ambalo ndilo mbaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya
taifa hilo.
Rais Mwai Kibaki ameagiza uchunguzi kamili kuhusiana na tukio hilo.
Bwana Kavulundi amesema kuwa mkuu wa polisi
mkoani humo John M'Mbijiwe, afisa mkuu wa kitengo cha polisi cha
kupambana na wezi wa mifugo ASTU Remi Ngugi na afisa mkuu wa polisi
wilayani Njoro Peter Nthiga wamesimamishwa kazi.
Amesema watatu hao huenda wakahujumu uchunguzi ikiwa wataendelea kusalia madarakani.
Joshua Waiganjo amesemekana kuwafuta kazi na kuwaajiri maafisa wengine wa polisi katika mkoa wa Rift Valley wakati huo.
Baada ya kukana mashtaka hayo, kesi hiyo
ilihairishwa ili kumruhusu mshukiwa huyo kutafuta matibabu kutokana na
ugonjwa wa kisukari katika hospitali moja nchini humo.
No comments:
Post a Comment