KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
jana aliwekwa kiti moto na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha
(IFM), wakilalamikia kiteno cha polisi kutowachukulia hatua watuhumiwa
waliowadhalilisha wanafunzi wenzao kwa kuwaingilia kinyume cha maumbile
na kuwaibia mali zao.
Wanafunzi hao ambao waliandamana kutoka kwenye hosteli zao eneo la
Kigamboni hadi makao makuu ya Jeshi la Polisi, walilazimika kuongozana
na Kamanda Kova hadi kwenye makazi yao, hivyo akawaahidi kufuatilia na
kuwafichua vibaka hao.
Akizungumza na wanafunzi hao kwenye viwanja vya Machava, alisema zoezi
hilo la kuwafichua vibaka hao litawahusisha wanafunzi watatu
wakishirikiana na polisi watatu, ambao watafanya kazi takriban wiki
mbili na kutoa ufafanuzi Januari 30, mwaka huu.
Wanafunzi hao walidai kulawitiwa, kuibiwa kompyuta mpakato 300 pamoja
na fedha taslimu ambazo hazijafahamika thamani yake hadi sasa.
“Mosi nasikitika taarifa hizi kuzipata juzi, hivyo nawaahidi
kuzishughulikia kikamilifu kwa kuwa matukio hayo hayajaripotiwa, ni bora
yaripotiwe polisi sasa ili hatua za haraka zichukuliwe,” alisema Kova.
Rais wa wanafunzi wa chuo hicho, Michael Charles, alieleza kuwa mbali
na ukatili wa vitendo hivyo, Kituo Kidogo cha Polisi cha Kigamboni
kimeshindwa kuyatatua matatizo hayo na kuwafichua vibaka hao wakati
orodha yao inafahamika.
Alisema wanafunzi waliofanyiwa ukatili wa kulawitiwa hadi sasa ni
wawili huku wengine walipigwa na kuumizwa sehemu mbalimbali za miili
yao.
Wakati huo huo, mtoto Abdallah Mohamed (9), naye aliahidi kufichua maficho ya vibaka hao kwani anawafahamu.
Maandamano ya wanafunzi hao yalianzia Ofisi za Wizara ya Mambo ya
Ndani na kupiga kambi Kivukoni, ambapo yalidumu kwa saa kadhaa kabla ya
Jeshi la Polisi kuingilia kati.
No comments:
Post a Comment