MADIWANI jijini Dar es Salaam, wameomba kikao cha dharura na
Meya wa Jiji, Dk. Didas Masaburi, kutokana na kushitushwa na hatua ya
kubadilishwa kwa jina la Benki ya Wananchi wa Dar es Salaam.
Wakizungumza baadhi ya madiwani wa Manispaa
ya Ilala na Kinondoni, walieleza kushangazwa na uamuzi uliofikiwa na
bodi ya benki hiyo kuamua kuibadili jina benki hiyo na kuwa Dar es
Salaam Commercial Bank.
Diwani wa Saranga, Ephraim Kinyafu, alisema wameshangazwa na
kubadilishwa kwa jina hilo huku wakishindwa kuwashirikisha viongozi hao
ambao ni wawakilishi wa wananchi, hatua inayowafanya wahitaji kikao cha
dharura na meya wa jiji.
Naye Diwani wa Segerea, Azurly Mwambaja, alisema benki hiyo
ilianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa jiji hilo hivyo kulikuwa
na umuhimu wa kujua faida iliyopatikana kabla ya kuhamia katika jina
jingine la kibiashara.
Mmoja wa madiwani ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu
hakupenda jina lake litajwe, alisema kuwa ili manispaa kuendelea kuwepo
katika bodi wanatakiwa kuchangia sh bilioni 1.2, jambo ambalo
linaonekana kushindwa kutekelezwa.
“Ni lazima tufike mahali tuseme hapana, kwani manispaa tatu za jijini
ndizo zilizoanzisha benki hiyo kwa mtaji wa sh milioni 500, leo unataka
tuchangie fedha ili tuendelee kuwapo katika bodi na kuwa wanahisa, kwani
hiyo benki tangu imeanzishwa haijapata faida?” alihoji.
Akizungumzia hilo, Meya wa Jiji, Dk. Masaburi, alikiri kubadilishwa
jina kwa benki hiyo na kusema walishirikishwa wanahisa wote kwa kufuata
katiba.
“Sijapata taarifa ya madiwani kuhitaji kikao bali ninachofahamu ni
kuwa niliwasikia sikia baadhi ya madiwani wakiongea katika kikao cha
madiwani cha jiji…kama watahitaji kikao basi nitakiitisha ili
tuzungumze,” alisema.
No comments:
Post a Comment