Huduma za simu za mkononi zinazofahamika kama "Apps" zinapata watumiaji
wengi Afrika, ambapo wanafunzi wawili wa teknolojia ya habari wa Uganda
wamebuni App inayoonyesha mahali pa kununua mafuta ya gari.
Edward Sekeywa anaendesha gari lake mjini Kampala. Tangi lake la mafuta
linakaribia kuwa tupu na hivyo ni lazima aharakishe kwenda kununua
mafuta. Lakini mafuta hayo yanauzwa kwa bei ghali mjini Kampala. Hata
hivyo, bei zinatofautiana kutoka kituo kimoja cha mafuta hadi kingine.
Ili kufahamu mahali atakapoweza kununua mafuta kwa bei nafuu, Edward
anaitazama simu yake ya mkononi.
Edward Sekeywa anaanza safari. Ana umri wa miaka 40 na ni mmoja wa watu
wa tabaka la kati linaloongezeka nchini Uganda. Bw. Sekeywa anafanya
kazi katika shirika lisilo la kiserikali. Anamiliki gari aina ya
Volkswagen na nyumba na ana mtoto mmoja tu. Ingawa anapokea mshahara
mzuri, Sekeywa anaeleza kwamba ni lazima atumie fedha yake kwa busara.
Anapofika kwenye kituo cha mafuta, anashtuka.
"Hili ni jambo la ajabu. App hii ilinionyesha kwamba bei ya mafuta ni
shilingi 3,350 lakini hapa bei ni 3,600. Samahani bwana. Hujambo? Mafuta
yanauzwa shilingi ngapi? Sawa, basi nitachukua ya shilingi 20,000.
Ameniambia kwamba kwa mara ya mwisho walikuwa na bei ya 3,350 wiki moja
iliyopita."
"Mafuta-Go"
Edward Sekeywa akitafuta mafuta ya bei rahisi.
Mafuta yanauzwa kwa bei ghali Uganda. Ingawa hakuna kodi inayotozwa,
mafuta hayo ni lazima yasafirishwe hadi bandari ya Mombasa na kisha
kuchukuliwa kwa magari maalum na hatimaye kufikishwa kwenye vituo vya
uuzaji. Hivyo, gharama ya usafirishaji ndiyo inayoifanya bei ya mafuta
iwe juu.
Hivyo ni muhimu mtu alinganishe bei, kabla ya kulijaza gari lake mafuta.
Hilo ni jambo lililogunduliwa mapema na wale walioubuni huduma ya
kulinganisha bei za mafuta.
Christine Ampaire na Daniel Odong ni wanafunzi wa teknolojia ya habari.
Wanaeleza kwamba mwaka moja uliopita walianzisha kampuni yao walioipa
jina la Code-Sync. App yao iitwayo Mafuta-Go ni ya bure na inaweza kutumiwa na kila mtu. Ampaire na Odongo waliweza kugharamia utengenezaji wa App hiyo kwa fedha walizoshinda katika shindano Pivot East la kubuni Apps za simu za mkononi.
Wavumbuzi wa "Mafuta-Go"
Wavumbuzi wa "Mafuta-Go", Christine Ampaire na Daniel Odongo.
Ampaire na Odongo waliweza kujinyakulia zawadi ya dollar za
Kimarekani 10,000. Hivi sasa watumiaji wa App ya Mafuta Go wanaweza pia
kupata taarifa juu ya mahala panapouzwa mafuta kwa bei rahisi kupitia
ujumbe unaotumwa katika mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter.
"Tunajitahidi sana kuwa na ushirikiano na vituo vya mafuta ili programu
ya Mafuta Go iweze kujazwa taarifa kutoka vituo hivyo moja kwa moja.
Lakini hivi sasa inabidi kila asubuhi tumtume mtu na pikipiki kwenda
kuchunguza bei za mafuta katika vituo vya Kampala." Christine Amapire
anaelezea mipango yao ya baadaye.
Mbali na kuwaonyesha watu bei mkatika vituo vya mafuta, App ya Mafuta go
inamwarifu pia mtumiaji wake iwapo kituo fulani kimeishiwa kabisa
mafuta.
No comments:
Post a Comment