Zaidi
ya abiria 1,000 wa treni ya Shirika la Reli nchini (TRL), jana
walikwama katika stesheni ya Dodoma baada ya mataluma ya reli kuzolewa
na mvua katika vituo vya Godegode na Kidete mkoani humu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya abiria wa
treni hiyo walisema walifika Dodoma saa 9:00 usiku kuamkia jana
wakitokea Bara kuelekea jijini Dar es Salaam.
Mariam Hassan, mmoja wa abiria kutoka Kigoma, alisema walijulishwa
na uongozi wa TRL kuwa mataluma ya reli yamezolewa na maji ya mvua
hivyo hakuna uwezekano wa kuendelea na safari hadi hapo eneo hilo
litakapofanyiwa matengenezo.
“Kibaya zaidi kinachotusikitisha ni kuwa eneo hilo limekuwa ni kero
kwa usafiri wa gari moshi kwa muda mrefu lakini serikali
hailishughulikii ipasavyo na kusababisha wananchi kupata shida kama
hii,” alisema.
Alisema baadhi yao wameishiwa fedha za chakula kwa kuwa
walitegemea kuwasili jijini Dar es Salaam jana kulingana na ratiba ya
treni hiyo.
Aliongeza kuwa hali hiyo imewafanya abiria hao sasa kugeuka
ombaomba. Abiria mwingine, Maduka Mwanang’ayo, kutoka Mpanda, alisema
kukwama kwa gari moshi katika kituo hicho cha Dodoma kumewasababishia
kero nyingi.
Alizitaja kero hizo kuwa ni huduma za choo ni za kulipia katika kituo hicho pamoja na bei ya vyakula kupanda holela.
“Tangu tumefika hapa usiku tulitangaziwa kuwa haturuhusiwi
kujisaidia kwenye vyoo vilivyopo ndani ya gari moshi hivyo huduma hizo
zinapatikana kwa kulipia katika vyoo vilivyopo katika kituo hicho na
abiria takayekutwa akijisaidia pembeni mwa gari moshi, atatozwa faini ya
Shilingi elfu thelathini,” alisema.
Naye Stesheni Masta wa Stesheni ya Dodoma, Flavian Nyawale,
akizungumza na waandishi wa habari, alisema kukwama kwa gari moshi hilo
kumetokana na mataluma ya reli kuzolewa na maji juzi katika vituo vya
Godegode na Kidete.
Nyawale alisema gari moshi lililokwama kituoni hapo lilikuwa likitoka Mwanza, Kigoma na Mpanda.
Alisema baada ya gari moshi hilo kufika Stesheni ya Dodoma,
walipata taarifa kuwa mataluma ya reli yamezolewa na maji ya mvua eneo
la Godegode na kwa msingi huo isingewezekana kuruhusu liendelee na
safari. Alisema mafundi wa shirika hilo wanaendelea kulifanyia
matengenezo eneo hilo na wanatarajia yatakamilika mapema na walitarajia
kuliruhusu garimoshi hilo kuendelea na safari zake jana 2:00 usiku.
Kuhusu kero wanazozipata abiria waliokwama katika stesheni hiyo, alisema shirika hilo limewapa Sh. 4,000 za chakula kila abiria.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment