MAGOLI
mawili ya Kevin-Prince Boateng na Sulley Muntari yameipa ushindi mnono
AC Milan dhidi ya Barcelona katika mchezo wa kusisimua wa Ligi ya
Mabingwa Ulaya.
Kwa ushindi huo wa nyumbani, AC Milan imejiweka pazuri katika mchezo wa marudiano wiki tatu zijazo.
AC
Milan walikuwa na kazi kubwa ya kutibua mipango ya washambuliaji wa
Barcelona kabla ya wachezaji hao wawili raia wa Ghana waliowahi
kuichezea Portsmouth ya Uingereza kufunga katika kipindi cha pili.
Boateng alijikunjua na kuachia shuti lililojaa wavuni dakika ya 57 baada ya kuufumania mpira ulizozagaa kabla ya Muntari hajafunga kwa shuti la karibu dakika ya 81 likiwa ni goli lake la kwanza katika Ligi ya Mabingwa.
Kilikuwa ni kiwango cha hali ya juu kilichoonyeshwa na wenyeji kilichozima kabisa ubunifu wa Lionel Messi.
Viungo
wa Milan Riccardo Montolivo na Massimo Ambrosini walihakikisha njia
zote zinazibwa na ushindi huo unawaweka kwenye nafasi nzuri ya kulipiza
kisasi cha kutolewa na Barcelona kwenye hatua ya robo fainali msimu
uliopita.
Katika msimu uliopita timu hizo zilitoka sare ya 0-0 San Siro na baadae Barcelona kushinda 3-1 katika mchezo wa marudiano.
Katika mchezo mwingine Galatasaray ya Uturuki ilitoka 1-1 na Schalke 04 ya Ujerumani.
No comments:
Post a Comment