Sheikh Ponda |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali
pingamizi la mawakili wa upande wa utetezi katika kesi inayomkabili
Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Sheikh Ponda na wezake.
Ponda na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya sh milioni 59.
Pingamizi hilo lilitaka mahakama hiyo isipokee kama kielelezo maelezo
ya ungamo yaliyotolewa na mshtakiwa wa tano katika kesi hiyo, Mkadamu
Swaleh Abdallah, wakati akiwa polisi.
Akipitia uamuzi huo Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa,
alisema imefikia uamuzi wa kulipokea ungamo hilo chini ya kifungu cha
169 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 licha ya ukweli kwamba
ungamo hilo limevunja matakwa ya kifungu cha 50(1)(a) kinachomtaka ofisa
wa polisi amchukue maelezo mshtakiwa ndani ya saa nne tangu
alipokamatwa lakini Mkadamamu alichukuliwa maelezo hayo masaa manne
yalikuwa yamepita.
“Licha ya mahakama hii kupokea kielelezo hiki ambacho kimeandaliwa nje
ya muda wa sheria unavyotaka lakini ieleweke kwamba kifungu cha 169 cha
Sheria ya Makosa ya Jinai, kinailazimisha mahakama kupokea kielelezo
cha aina hiyo ambacho kimezidisha muda kwani mahakama hii imeona
kuongezeka kwa masaa matatu nje ya muda wa sheria unavyotaka hakukuweza
kumshawishi mshtakiwa huyo kukiri makosa yake ndani ya ungamo.
Alisema ndani ya ungamo hilo, amekiri kutenda makosa yanayomkabili
likiwemo la kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Markas na
kwamba anapokea ungamo hilo kama kielelezo.
Uamuzi huo wa hakimu, ulitokana na pingamizi lililowasilishwa juzi na
mawakili wa utetezi, Juma Nassor, wakati shahidi wa nane wa upande wa
jamhuri Sajenti Mkombozi Mhando kuomba maelezo hayo ya onyo yapokelewe
kama kielelezo kwa sababu yamekidhi matakwa ya kisheria.
Baada ya uamuzi huo kutolewa saa 8:30 mchana, kesi kubwa ilianza
kusikilizwa ambapo shahidi wa tisa wa jamhuri Sajenti Juma alianza kutoa
ushahidi wake na kudai kuwa yeye ndiye mpelelezi wa kesi hiyo na kwamba
alipewa jukumu la kwenda kutembelea eneo la tukio la kiwanja cha
Chang’ombe Marks na kushuhudia uharibifu mkubwa uliokuwa umefanywa na
washtakiwa hao.
Wakati huo huo, Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Kipolisi Mkoa wa Dar es
Salaam (ZDCO), Hemed Msangi, ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi ya
kula njama na kufanya maandamano haramu inayowakabili Salum Bakar Makame
na wenzake 53 jana aliieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kati
ya Februari 11-17, mwaka huu, yeye alikuwa ndiye Kamanda wa Kanda ya
Maalumu ya Dar es Salaam na kwamba Februali 11 alipokea barua toka
Shura ya Maimamu iliyokuwa ikimuomba kibari cha kufanya maandamano ya
kwenda ofisini kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Alisema maandamano hayo yalikuwa na lengo la kuhoji kwa nini DPP
hatoi dhamana kwa Ponda na kwamba maandamano hayo yalikuwa yakitaka
yafanyike Februari 15 baada ya swala ya Ijumaa kutokea misikiti
mbalimbali.
KamishnaMsaidizi huyo wa Polisi, Msangi, alidai yeye na maofisa
wenzake walitafakari hiyo barua ambayo ilikuwa na saini ya Sheikh Juma
Idd ambaye ni Amir wa Shura ya Maimamu Temeke na walijiuliza uzito wa
maandamano hayo.
Alidai kuwa walibaini kwamba hawakuwa na askari wa kutosha wa
kuwapeleka kila msikiti kwa ajili ya kuyalinda maandamano hao, hivyo
hali hiyo isingekuwa rahisi kudhibiti maandamano hayo.
Alidai kuwa waliamua kuyazuia kwa sababu walibaini kuwa ofisi ya DPP
iko katikati ya jiji na ina sehemu finyu, hivyo kama yangeruhusiwa
yangeweza kuathiri haki za watu wengine wanaotumia jengo hilo la ofisi
ya DPP.
Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo juzi wakituhumiwa kufanya maandamano bila kibali.
No comments:
Post a Comment