SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), limezuia kufanyika kwa
Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hadi
litakapotuma wajumbe wake kuja nchini kupata ukweli wa malalamiko
yaliyowasilishwa kwao kuhusu uchaguzi huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF Leodegar Chilla
Tenga, alisema Jumapili alipata simu kutoka Fifa ikimjulisha kuwa
wamepokea malalamiko kutoka kwa mgombea mmojawapo akisema hakutendewa
haki na Kamati ya Rufaa.
Tenga alisema kwa vile tayari wajumbe watano walikuwa wamewasilisha
ombi Kamati ya Rufaa ipitie upya uamuzi wake wa kuwakata, aliieleza Fifa
isubiri hadi kamati hiyo itakapotoa maamuzi yake.
“Juzi (Jumapili), nilipata simu kutoka Fifa ikinieleza kuwa wamepata
malalamiko kuhusiana na mwenendo wa uchaguzi, wakataka maelezo yangu na
nikawaeleza kungekuwa na haja ya kutuma ujumbe ili wapate ukweli ili nao
waweze kutoa ushauri,” alisema Tenga na kuongeza: “Lakini nikaeleza
kuwa tayari Kamati ya Rufaa ambayo ni chombo cha mwisho kimaamuzi kwa
ngazi ya kitaifa, ingelikutana, nikawataka wanipigie jana jioni (juzi),
kweli jamaa wale kwa kuonyesha kujali, wakapiga kujua nini kimeamuliwa,”
alisema Tenga.
Alisema kwa mazingira yalivyo watakuja nchini katikati ya mwezi ujao
ambapo watakutana na walalamikaji, Kamati ya Rufaa chini ya Idd
Mtiginjola na wadau mbalimbali kulingana na mazingira ya jambo hilo kwa
lengo la kupata jawabu.
Tenga amesema ujio wa ugeni huo ni faraja kubwa kwake, shirikisho hilo
na soka ya
Tanzania kwani ukweli wa mambo utajulikana na kwa vile hicho
ni chombo cha juu katika soka, kutakuwa hakuna wa kuhoji.
Alisema kwa mazingira ya sasa ambapo baadhi ya wadau wanalalamika
kukatwa isivyo halali na kila mdau akiwa na mtazamo wake, ni vigumu
kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki kwani asingependa kuondoka
madarakani akiacha msigano na mgawanyiko.
“Tukifanya uchaguzi kwenye hali hii, ni kulipeleka soka kwenye
mgawanyiko, wamesema wataketi kuamua nini cha kufanya kabla ya kutuma
ujumbe nchini kuja kujua kiini cha tatizo ili kufanya maamuzi,” alisema
Tenga sentahafu wa zamani wa Yanga, Pan Africa na Taifa Stars.
Alisema ujio wa ujumbe huo wa Fifa, ni muhimu kwani ni kitu cha hatari
uongozi wa soka kuanza kazi kwenye mazingira ya mifarakano, akisema
raha ya uongozi ni kuanza kwa miguu yote ikiwemo baada ya zoezi la
uchaguzi watu wakapongezana.
Tenga aliyekalia kiti hicho kwa mara ya kwanza Desemba 27, 2004,
alisema kwa mazingira hayo, Fifa wametaka mkutano mkuu usifanyike hadi
watakapokuja na kuyapatia ufumbuzi malalamiko yaliyowasilishwa kwao na
wadau.
Kwa mazingira hayo, Tenga amewasihi wajumbe wa mkutano mkuu wa
shirikisho hilo kuwa na subira kwa vile Fifa, wenye mchezo wao,
wamesitisha mchakato mzima wa uchaguzi huo.
Kuhusu hatma ya uongozi wake baada ya agizo hilo la Fifa, Tenga
alisema hakuna namna nyingine isipokuwa uongozi wake kuendelea hadi
uchaguzi mkuu utakapofanyika kwani kwa mujibu wa katiba ya shirikisho
hilo hakuna nafasi ya kamati ya muda.
Alipoulizwa kuhusu hatua ya Mtiginjola kugoma kupitia upya uamuzi wake
dhidi ya wagambea watano waliokuwa wameomba hivyo, Tenga alisema
anaheshimu uamuzi wa kamati hiyo kwani ndio ya mwisho kwa ngazi ya taifa
na hakuna msigano.
Awali Jamal Malinzi aliyekuwa akiwania nafasi ya urais katika
shirikisho hilo na wengine watano na kuchujwa na Kamati ya Rufaa,
waliwasilisha ombi kwenye kamati hiyo kupitia upya uamuzi wake, lakini
kamati hiyo ikagoma kwa hoja ya kufungwa mikono kisheria.
Wadau wengine ambao waliomba kupitiwa upya kwa uamuzi dhidi yao ni
Hamad Yahya aliyekuwa akiwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu na
waliokuwa wakiwania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ni Eliud
Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na
Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).
Hii ni kama ilivyokuwa kuelekea uchaguzi wa Desemba 27, 2004 ambapo
Crescentius Magori aliyekuwa amechujwa kwa kigezo cha kukosa uzoefu
katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini akarejeshwa na Fifa
kupitia kwa Ashford Mamelody na Joseph Mitsufield.
No comments:
Post a Comment