TAASISI ya Utawala Bora Tanzania (CEGODETA), imeiomba serikali
kukipiga marufuku kikundi cha Uamsho na jumuia ya kimataifa itangaze
kuwa ni kikundi hatari.
Kauli hiyo ilitolewa na mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Thomas
Ngawaiya, kufuatia kuzuka kwa matukio ya mauaji na uharibifu wa mali kwa
mgongo wa dini huko visiwani Zanzibar, huku kikundi hicho kikihusishwa
kwa ukaribu.
“Kwa kuzingatia hilo CEGODETA, tunaunga mkono tamko lililotolewa na
Rais Jakaya Kikwete kwamba uchunguzi wa kina ufanyike ambao
utashirikisha mashirika ya nje na wote wanaohusika na mauajji hayo
pamoja na wanaofadhili watu wao wachukuliwe hatua za kisheria ili kukata
mzizi wa fitina,” alisema.
Ngawaiya aliwatahadharisha Watanzania kutokubali kugawanywa kwa
misingi ya dini, ambazo zimeangamiza maisha ya watu wengi katika nchi za
Kiislamu duniani.
“Mabomu yamewahi kuua mamia ya watu huko Kenya, Uganda na Sudan kwa
sababu ya udini, hadi leo vurugu hizo za mauaji zinaendelea huko kwa
kasi.
“Kama Watanzania tusipokuwa makini mambo yaliyotokea kwenye nchi hizo
yaweza kutokea hapa kwetu, kwa asiyejua kufa mwambie akatazame kaburi,”
alisema.
Aidha aliitaka serikali itoe ulinzi wa kutosha kwa makanisa na
viongozi wote wa Kikristo huko Zanzibar, sambamba na bara, pia kwa
misikiti na viongozi wa misikiti wanaotishiwa maisha.
yaaniinasikitisha sana sijui tunaelekea wapi/
ReplyDelete