Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa BAHAKITA, Said Mwaipopo, alisema BAHAKITA kwa kushirikiana na taasisi ya Islamic Peace Foundation, hawaungi mkono maandamano hayo yaliyoratibiwa na Shuhura ya Maimam.
“Tunawataka Waislamu wote nchini wajiweke kando kabisa kuhusu maandamano hayo yanayoratibiwa na Shuhura ya Maimum, kwani hayana kibali chao polisi. Sisi hatuungi mkono kwani wanatakiwa kufuata sheria za nchi,” alisema Mwaipopo.
Mwaipopo alisema, Serikali na Mahakama wanajua wanachofanya, hivyo hawawezi kuendeshwa kwa shinikizo la watu wachache wanaotumiwa na wanasiasa kwa faida zao binafsi.
“Sisi hatufurahii kuona Ponda yuko ndani, ila tunachokitaka ni Waislamu wenzetu wafuate sheria, maana sisi tuna mpango wa kwenda kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, mratibu wa maandamano hayo achukuliwe hatua kwani ni mtu anayetumika kuchafua hali ya hewa ya nchi,” aliongeza.
Naye Mwenyekiti wa Peace Foundation, Sadi Godogodi, alisema hawaungi mkono maandamano hayo kwani ni kinyume cha sheria. Alisema maandamano hayo yanawaonesha Waislamu kuwa ni watu wa fujo na wasiotaka kufuata utawala wa sheria.
Wakati huo huo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewataka Waislamu kuwa watulivu na kutotumia nguvu kwa hali yoyote katika matatizo yanayogusa hisia za kiimani.
Taarifa hiyo ilitokana na kikao maalumu cha Baraza la Ulamaa chini Mwenyekiti wake, Mufti Sheikh Issa Bin Shabani Simba, kujadili vurugu za Waislamu na Wakristo katika Kijiji cha Buseresere, wilayani Chato mkoani Geita.
Baraza hilo limepokea taarifa hiyo kwa masikitiko na kutaka Waislamu kuwa wavumilivu na kutafuta njia bora ya kuweza kupata mwafaka kutatua mgogoro huo.
Baraza hilo litatuma ujumbe wake haraka kwenda Buseresere kufuatilia mambo yaliyojitokeza ili kupata ukweli uliosababisha vurugu hizo na kuchukua hatua kurejesha amani baina ya Waislamu na Wakristo.
No comments:
Post a Comment