WIZARA ya Kazi na Ajira, imeshindwa kutoa ufafanuzi kuhusu raia
wa kigeni wanaoishi nchini na kufanya kazi za kawaida ambazo kisheria
zinapaswa kufanywa na wazawa.
Katika mkutano kati ya wizara na waandishi wa habari jana, iliibuliwa
hoja ya kwanini wageni wanaajiriwa kwenye baadhi ya mahoteli makubwa na
makampuni kufanya kazi hizo za kawaida.
Licha ya kukiri kuwepo hali hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa wizara hiyo,
Ally Msaki, alijitetea kuwa wageni hao wamekuwa wakiwapatia vibali hivyo
kutokana na elimu zao.
Hata hivyo, utetezi huo unakuja wakati wizara hiyo pamoja na Idara ya
Uhamiaji zikilalamikiwa kutoa vibali vya makazi na kazi kwa wageni bila
kuzingatia sheria ambazo zimeainisha bayana kuwa wageni wanaruhusiwa
kufanya kazi za kitaalamu tu.
“Ni kweli wapo wengi, lakini hii ni kwa sababu tu ya vyuo wanavyotoka
kuwa na utaalamu zaidi, maana huko wanasomea masuala kama uchuaji wa
mwili, sidhani kama kwa nchini utaalamu huo upo. Hiyo ndiyo sababu ya
kuajiri watu kama hao kutoka nje,” alisema Msaki.
Awali, Msaki alisema kuwa ajira imeongezeka kwa kiwango cha 85,577
sawa na asilimia 6.7 kwa mwaka 2011 kutoka ajira 1,276,982 kwa mwaka
2010 hadi 1,362,559.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, takwimu hizo zimeandaliwa na wizara
yake sambamba na ofisi ya takwimu ambapo utafiti huo umeonesha kuna
ongezeko la ajira za masharti ya muda mrefu 82,969 sawa na asilimia 97
ya ajira zote.
Alisema utafiti umeonesha kuna uwiano kati ya ajira za wanawake
ukilinganisha na wanaume, ambapo umeongezeka kufikia asilimia 37.7 ya
ajira zote kutoka asilimia 36.5 mwaka 2010 na kwamba idadi ya wanaume
imeshuka hadi kufikia asilimia 62.1 ya ajira zote
kutoka asilimia 63.5
mwaka 2010.
Katika takwimu hizo, Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza katika kuajiri
watu wengi katika sekta rasmi ambapo jumla ya watu 456,815 sawa na
asilimia 33.5 kati ya 1,362,559 wameajiriwa.
Kwa mwaka wa fedha 2011/2012 jumla ya ajira 250,678 zilizalishwa
kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ni pamoja na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) ajira 34,516, Mamlaka ya Maeneo Huru Kiuchumi
(EPZA) ajira 15,100 na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) ajira
82,834.
No comments:
Post a Comment