KAMISHNA Msaidizi Mwandamizi wa Polisi aliyekuwa anasimamia
ajira katika jeshi hilo nchini, Renatus Chalamila amepewa likizo ya
mwezi mmoja baada ya kutajwa mara nyingi kuhusika kuwatoza fedha vijana
walioomba ajira za uaskari.
Wakati Chalamila akingoja uamuzi wa rais, maofisa wengine wanne wa
jeshi hilo wamesimamishwa kazi na wanatarajia kufunguliwa mashtaka ya
kijeshi kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukaji wa maadili na
taratibu za jeshi hilo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.
Emmanuel Nchimbi katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam, akisema kuwa Chalamila amepewa likizo hiyo na mapendekezo
kupelekwa kwa rais ili afanye maamuzi juu ya tuhuma zinazomkabili.
Alisema kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi limelazimika kuwaondoa
katika mafunzo askari wanafunzi 95 waliokuwa wamejiunga na chuo cha
polisi baada ya kubainika kuwa walipata fursa hiyo kwa kutoa fedha.
Kuhusu tuhuma za maofisa wengine, Waziri Nchimbi aliwataja
waliosimamishwa kuwa ni Elias Mwita aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa
Mbeya, msaidizi wake Jacob Kiango na aliyekuwa mkuu wa kikosi cha
kutuliza ghasia (FFU) wa mkoa huo, Charles Kinyongo.
Alisema kuwa maofisa hao walisimamishwa kazi tangu jana kutokana na
kukiuka maadili ya jeshi hilo, wakituhumiwa kupeleka chumvi na sukari
kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu badala ya kilo 1.9 ya dawa za kulevya aina
ya cocaine zilizokamatwa na askari mkoani Mbeya, Machi mwaka jana.
Kwamba dawa hizo zilikamatwa katika kituo cha Tunduma kisha
zikathibitishwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa kweli ni
mihadarati.
Waziri Nchimbi alisema vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya
viongozi wa jeshi vinawavunja moyo na kuwapa hofu askari wa ngazi ya
chini ambao hushindwa kufanya kazi zao kwa uadilifu unaotakiwa.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoani Kagera,
Peter Matagi amesimamishwa kazi na atafunguliwa mashtaka ya kijeshi
kutokana na kukiuka taratibu za kazi kwa kuwabambikiza kesi zisizo na
dhamana wananchi 13 wa Kata ya Nyakasimbi wilayani Karagwe.
Hatua hiyo ni kutokana na vurugu za kugombea ardhi ambazo hazikuwiana
na aina ya mashtaka waliyoshtakiwa hali inayoonesha dalili ya uwepo wa
rushwa.
Waziri Nchimbi alisema wananchi hao walibambikizwa kesi ya ujambazi
wa kutumia silaha ambapo walikaa mahabusu kwa muda wa miezi miwili na
baadaye timu ya uchunguzi iliyoongozwa na waziri mwenyewe iligundua
kuwa mashtaka waliyoshtakiwa hayakuwa sahihi hali ambayo ilisababisha
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) afute kesi.
Aliongeza kuwa serikali pia imemsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa
Polisi Wilaya ya Serengeti, Paul Mng’ong’o kwa kosa la kuingia katika
hifadhi ya mbuga za wanyama ya Serengeti na kupanga njama ya kuchimba
madini aina ya dhahabu hali iliyosababisha kushtakiwa kwenye mahakama
ya kiraia.
Waziri Nchimbi alitoa wito kuwa serikali itawaunga mkono askari
wanaofanya kazi kwa uadilifu ila watakaoenda kinyume na maadili na
taratibu haitasita kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafukuza
kazi.
No comments:
Post a Comment