RAIS Jakaya Kikwete ameombwa kuchukulia kwa uzito vitendo vya
timuatimua wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma kutokana na wanafunzi
hao kudai haki wanazopaswa kuzipata wawapo vyuoni.
Msemaji wa Umoja wa Wanafunzi waliofukuzwa katika Vyuo Vikuu nchini
(UUEST), Philipo Mwakibingwa, alitoa kauli hiyo jana wakati wa
uzinduzi wa umoja huo na kusema kuwa lengo kubwa la umoja huo ni
kutetea wanafunzi waliofukuzwa.
Alisema tangu miaka ya 2000 hadi sasa, suala hilo limezidi kukua
nchini, watawala wa vyuo vikuu ambao ni maprofesa na baadhi ya viongozi
waliopo serikalini kulichukulia kama mila na desturi.
Mwakibingwa alisema wanafunzi hao wamekuwa wakifukuzwa kutokana na
kutoa mawazo mbadala, kuhoji mambo, kukosoa uovu uliopo na unaondelea
kutendeka ndani ya vyuo, hivyo na kutoa ushauri pale inapobidi kwa
masilahi ya taifa lao.
Akizungumzia umoja huo, alisema wamefikia hatua ya kuunda umoja huo
kutokana na serikali pamoja na Bunge kushindwa kutatua matatizo yao na
kuongeza kuwa hali hiyo imesababishwa na taarifa potofu zilizotolewa na
watawala wa vyuo vikuu hivyo.
“Kwa sababu watawala wa vyuo vikuu wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kututenganisha na jamii zetu, familia zetu, jamaa, viongozi wetu wa
kidini na asasi kwa taarifa za uongo kupitia vyombo vya habari, tumeona
suluhu ya maisha yetu ni kuungana. Muungano huu umeundwa kwa ajili ya
kutetea maisha yetu,” alisema Mwakibingwa.
No comments:
Post a Comment