Azam FC inafahamu kwamba ina fursa kujisafishia njia ya kucheza
hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hilo litawezekana
ikiwa itaibuka na ushindi leo dhidi ya timu imara ya maafande wa FAR ya
Morocco.
Mtanange huo baina ya wawakilishi hao pekee wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa na Waarabu hao litapigwa kuanzia saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam inayohaha kutaka kuandika historia mpya ya michuano hiyo licha ya kwamba inashiriki kwa mara ya kwanza, itaingia uwanjani ikijivunia kasi yake ya kuridhisha katika mechi zilizotangulia.
Matokeo ya ushindi wa jumla ya mabao 8-1 dhidi ya Al Nasri ya Sudan Kusini, kisha ule wa mabao 2-1 dhidi ya Barack Young Controller II ya Liberia ni wazi yatatumiwa kama kichocheo cha kuizamisha FAR leo.
Kocha wa Azam Stewart Hall amewataka washambuliaji
wake wahakikishe wanatumia nafasi kikamilifu kwa kufunga mabao kadri
inavyowezekana.
Pamoja na hilo, Hall amewataka mabeki wake wawe makini ili waweze kuepusha madhara yanayoweza kuikabili timu yake kutokana na mashambulizi ya kushtukiza ya FAR.
“Sisi tutacheza mfumo wetu ule ule wa 4-4-2,
tukimiliki mpira muda mwingi na kufanya mashambulizi ya kusaka mabao kwa
tahadhari tukijihami na mbinu ya wapinzani wetu kutushambulia kwa
ghafla,” alisema Hall.
Hall huenda akampumzisha mshambuliaji Brian Umony ambaye kwa mujibu wa mazoezi ya timu hiyo anaonekana kutokuwa fiti licha ya kwamba alicheza mechi dhidi ya Barrack.
Naye kocha wa FAR Ouadani Lahcen amesema hana
ufahamu wa kutosha na Azam, lakini yuko tayari kuikabili na kuvuna
ushindi akitumia mbinu ‘alizoiba’ kutoka Timu ya Taifa (Taifa Stars).
Hata hivyo, Azam itabidi iwe makini na safu yake ya ulinzi ambayo imekuwa ikiyumba katika michezi yake ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Safu ya ulinzi ya timu hiyo inaongozwa kipa,
Mwadin Ally, beki wa kati na David Mwantika na Joaqins Atudo wakati
mabeki wa pembeni wanacheza Himid Mao na Wazir Salum.
Nafasi hiyo ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa mengi kutokana na mara nyingine kutoelewana na hivyo kuruhusu mabao ya kizembe.
No comments:
Post a Comment