SERIKALI imetenga sh trilioni 4.7 kwa ajili ya nyongeza ya
mishahara na kugharimia mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu,
Serikali za Mitaa na Wakala wa Taasisi za Serikali.
Hata hivyo, serikali imeshindwa kutaja kiasi cha nyongeza hiyo na
badala yake imetaja kiasi cha jumla kilichotengwa kwa ajili ya nyongeza
ya mishahara na stahiki nyingine.
Kiasi hicho ni tofauti na mwaka wa fedha uliopita 2012/13 ambapo
ilitenga sh trilioni 3.7 huku mshahara wa kima cha chini ukiongezeka
kwa sh 20,000.
Ongezeko hilo lilifanya mshahara wa kima cha chini uongezeke kutoka sh 150,000 hadi sh 170,000.
Nyongeza hiyo ya mishahara ilitangazwa jana na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, wakati
akiwasilisha makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2013/14.
“Kiasi hiki cha sh trilioni 4.7 kitatumika kugharamia ajira mpya,
upandishwaji vyeo na nyongeza za kawaida za mishahara za mwaka pamoja
na nyongeza za mishahara kuanzia Juni 2013,” alisema.
Waziri Kombani alisema wizara yake itasimamia ajira za watumishi wa
umma ambapo katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kuajiri
watumishi wapya 61,915.
Alitaja sekta zitakazotoa ajira na idadi yake kwenye mabano kuwa ni
pamoja na walimu (33,586), Afya (11,221), Kilimo (1,604), Mifugo
(2,500) na watumishi wengine 12,804.
Kwa mujibu wa Waziri Kombani, watumishi 42,419 wa kada mbalimbali watapandishwa vyeo.
Katika mwaka huu wa fedha, Waziri Kombani alisema serikali imeandaa miongozo ya maadili katika utumishi wa umma.
Alisema kuwa miongozo hiyo ni nyenzo ya kuhakiki tabia na mienendo ya
watumishi wa umma na nyenzo ya kuongeza tija na kuhakikisha matumizi
bora na sahihi ya rasilimali fedha, vitu na watu.
“Serikali haitasita kuwachukulia hatua stahiki watumishi wasio
waadilifu, wasio wajibika na wale wote wanaojihusisha na vitendo
vinavyosababisha matumizi mabaya ya madaraka na mali za umma,” alisema.
Waziri Kombani aliliomba Bunge liidhinishe sh bilioni 9.2 kwa ajili
ya Ofisi ya Rais Ikulu, sh bilioni 242.7 kwa ajili ya Ofisi ya Rais,
Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.
Aidha, aliomba sh bilioni 42.8 kwa ajili ya Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, sh bilioni 9.2 kwa ajili ya Ofisi ya Rais,
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi na sh bilioni 2.9 kwa ajili ya
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma.
Pia aliomba sh bilioni 11 kwa ajili ya Tume ya Utumishi wa Umma na sh
bilioni 2.2 kwa ajili ya Bodi ya mishahara na masilahi katika utumishi
wa umma.
No comments:
Post a Comment