SHULE 10 wilayani Ruangwa, Lindi, hazina vyoo baada ya kubomoka kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Rueben
Mfune, alibainisha hayo juzi wakati akisoma taarifa katika kikao cha
Baraza la Madiwani cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2012/2013
kilichofanyika katika Soko la Tasaf wilayani hapa.
Alizitaja shule hizo za msingi kuwa ni Mtakuja, Mbecha, Namihegu,
Mpumbe, Mtawile, Nanjaru, Chienjere, Ruangwa, Dodoma na Mandawa, ambazo
zipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Mfune alisema kutokana na maafa hayo mpaka sasa hatua zilizochukuliwa
ni kuchimba vyoo vya muda katika maeneo husika kwa kushirikisha
wananchi.
“Hatua tunayolenga kuchukua sasa ni kununua vifaa vya ujenzi na
tathmini ikikamilika itapelekwa kwenye kamati ya fedha na uongozi kabla
ya utekelezaji,” alisema Mfune.
Mfune alisema kuwa utekelezaji wa kazi hiyo utakuwa kati ya Juni
mwaka huu na watatumia fedha zilizotengwa kuwezesha miradi ngazi za
chini kutatua jambo hilo la dharura.
Pamoja na mambo mengine yaliyojili ndani ya kikao hicho, madiwani hao
walichachamalia malipo ya korosho na kuitaka serikali kuwalipa
wananchi malipo yao ya pili ya korosho.
“Wananchi wamekuwa wakitunyoshea vidole tunapokwenda vijijini katika
shughuli zetu za kikazi na tumekuwa tukiwaambia hali halisi ya
ucheleweshaji wa malipo yao, lakini wao wamekuwa hawatuelewi, wao
wanataka hela zao.
“Kwa kweli tunahatarisha maisha yetu, kwani wamekuwa wakitutishia
maisha na sisi kama binadamu lazima tuogope yasije yakatokea kama
yaliyotokea kwa wenzetu wabunge wa Mkoa wa Mtwara kuchomewa nyumba zao
moto,” walisema madiwani hao.
Diwani wa Matambalale, Omary Liwikila (CUF), alitaka mfumo wa
stakabadhi ghalani uondolewe, kwani unaleta usumbufu na ubabaishaji kwa
wananchi.
“Huu mfumo kwa upande wangu naomba uondolewe, kwani unaleta usumbufu
kwa wananchi. Wananchi wanalima kwa shida na wakati wa kuneemeka katika
kuuza mazao yao ya korosho wapate shida tena ya kudai dai malipo?”
alihoji Liwikila.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mfune, akijibu hoja
hiyo, alisema hawezi kutoa tamko juu ya suala hilo, hivyo wanasubiri
serikali yenyewe itakapoamua kuondoa mfumo huo wa stakabadhi ghalani.
No comments:
Post a Comment