VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga, jana ilizidi kuunusa ubingwa
baada ya kuwapigisha kwata maafande wa JKT Ruvu na kuwachapa mabao 3-0
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo, timu zote zilianza kwa kasi huku JKT ikimtumia
mshambuliaji wake Mussa Hassan Mgosi, kuliandama lango la Yanga kusaka
bao la mapema.
Dakika ya 34, Hamis Kiiza alishindwa kuitumia vema nafasi ya kufunga
baada ya shuti lake kutoka nje wakati kipa Shabani Dihile akiwa hayupo
langoni.
Alikuwa ni mshambuliaji mwenye kasi, Simon Msuva, dakika ya 45,
alipoanza kuzichana nyavu za JKT kwa bao safi akimalizia mpira
uliorushwa na Kiiza na kuwafanya wachezaji wa JKT kumzonga mwamuzi Oden
Mbaga wakililalamikia.
Kipindi cha pili, Yanga iliingia kwa kasi huku JKT wakionekana kuchoka
na kuwafanya vijana hao wa Jangwani wakitawala mchezo na dakika ya 58,
Kiiza alizidi kuwanyong’onyeza maafande hao, baada ya kupachika bao la
pili kwa kichwa akimalizia faulo iliyopigwa na David Luhende, baada ya
Msuva kuchezewa madhambi.
Yanga iliendelea kuliandama lango la JKT na dakika ya 64, Nizar
Khalfan alikamilisha mahesabu kwa kutupia kambani bao la tatu akimalizia
mpira wa Frank Domayo uliogonga mwamba na kurudi uwanjani. Hadi mwamuzi
Mbaga anamaliza mpira, Yanga iliibuka na ushindi huo wa 3-0.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 56 zinazoweza kufikiwa na
Azam pekee inayoifuatia ikiwa na pointi 43 wakati nafasi ya tatu ni
Kagera Sugar yenye pointi 40 huku JKT Ruvu ikibaki na pointi zake 23.
Sasa vijana hao wa Jangwani wamebakiza pointi moja tu kutazawa mabingwa wapya wa Soka Tanzania Bara.
African Lyon yenye pointi 19 sawa na Polisi Morogoro zinazoburuza
mkia, pamoja na Toto Africans yenye pointi 22 ziko kwenye hatari ya
kushuka daraja msimu huu.
Yanga: Ally Mustafa/Said Mohamed, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir
Haroub, Kelvin Yondani, Athumani Idd, Simon Msuva, Frank Domayo, Hamis
Kiiza/Jerry Tegete, Nizar Khalfan/Said Bahanuzi, Haruna Niyonzima.
JKT Ruvu: Shabani Dihile, Hassan Kikutwa/Sostenes Manyasi, Stanley
Nkomola, Madenge Ramadhani, Damas Makwaya, Nashon Naftar, Amos
Mgisa/Abdalllah Bunu, Ally Mkanga/Charles Thadeo, Musa Hassan Mgosi,
Zahoro Pazi, Haruna Adolf.
No comments:
Post a Comment