MKAZI wa Kivule, Dar es Salaam, Emmanuel Salagata (45-50) amejiua kwa kujinyonga baada ya kumchoma kisu shingoni mwanae.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minagi, alisema jana
Salagata alijinyonga juzi, majira ya saa 2 asubuhi maeneo ya Kitunda kwa
kutumia kamba aliyokuwa ameitundika kwenye dari chumbani kwake.
Alisema siku moja kabla ya tukio, Salagata akiwa kwenye kilabu ya
pombe kwa Mama Zawadi, alimchoma kisu shingoni mwanaye George Emmanuel
(30) ambaye alitibiwa katika Hospitali ya Amana na kuruhusiwa.
Kamanda Minagi alisema sababu za mzazi huyo kumchoma mwanaye kisu ni
katika hali ya ulevi na alipoona hivyo alijua amemuua mwanaye ndipo
alipoamua kujinyonga.
Kwa mujibu wa Minagi, marehemu aliacha ujumbe unaosomeka: “Nimejiua
kwa kujinyonga kwa amri yangu na kero za watu”. Mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakati huohuo, fundi ujenzi, Peter Salum (40) amekutwa chumbani kwake
akiwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya manila aliyoitundika
kwenye kenchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tukio
hilo lilitokea juzi majira ya saa 12:00 jioni maeneo ya Kimara
Mavurunza.
Sababu za kujinyonga bado hazijafahamika kwa kuwa marehemu hakuacha
ujumbe wowote. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala
kwa uchunguzi.
No comments:
Post a Comment