JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limemsimamisha uanachama kwa
muda usiojulikana, Mhariri wa Mtanzania Jumatano, Charles Mulinda, kwa
sababu za kukiuka maadili ya uandishi wa habari.
Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Jukwaa
hilo, Nevil Meena, alisema TEF imechukua uamuzi huo baada ya kupokea na
kujadili kwa kina taarifa ya kamati ndogo ya wahariri watatu ambayo
iliongozwa na Mhariri wa Nipashe, Jesse Kwayu, kwa ajili ya kuchunguza
habari iliyochapishwa na gazeti la Mtanzania, Jumatano Aprili 17, mwaka
huu ikiwa na kichwa kisemacho ‘Mtandao Hatari’.
Katika habari hiyo, Meena alidai kuwa iliwataja wahariri wawili,
Ansbert Ngurumo wa Tanzania Daima na Deodatus Balile wa Jamhuri kuwa ni
washirika wa Joseph Ludovick, mshitakiwa katika kesi ambayo ilikuwa
ikihusishwa na ugaidi (kabla ya kubadilishwa na mahakama) lakini
ikiwahusisha kwa namna moja au nyingine na tukio la kuumizwa kwa
Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda.
“Yalikuwa ni maoni ya wahariri wengi katika mkutano wa Aprili 18,
2013, kwamba habari hiyo ilikuwa na upungufu mkubwa kitaaluma, hivyo
kuamua kuchunguza habari hiyo na kubaini iwapo kulikuwa na ukiukwaji wa
maadili na misingi ya kitaaluma ya habari.
“Pamoja na mambo mengine ilipaswa kuchunguza mazingira ya kuchapishwa
kwa habari hiyo na kama kulikuwa na msukumo wowote nyuma ya kuandikwa
kisha kuchapishwa kwakwe,” alisema.
Meena alisema kamati hiyo ilipaswa kuchunguza ushahidi wa tuhuma
zilizotolewa dhidi ya Deodatus Balile na Ansbert Ngurumo (kama Mullinda)
alivyokiambia kikao cha Aprili 18 kwamba alikuwa na ushahidi wa yale
aliyoyaandika.
Aliongeza kuwa TEF ilibaini kulikuwa na ukiukwaji wa maadili ya
kitaaluma katika mchakato mzima uliowezesha kuandikwa na kuchapwa kwa
habari husika na kwamba habari hiyo haikuwa na sifa wala vigezo vya
kihabari.
Hata hivyo, Meena alisema Mulinda alipotakiwa kutoa ushahidi wa tuhuma
dhidi ya wahariri aliowataja, alishindwa kuthibitisha usahihi wa
taarifa hiyo.
Kwa kuzingatia matokeo hayo TEF inaushauri uongozi wa New Habari
(2006) Ltd na vyumba vingine vya habari kuboresha mfumo wake wa
usimamizi wa uhariri ili kuziba mianya kwa habari tata kama hiyo ya
‘Mtandao Hatari’ kupenya na kuwaumiza baadhi ya watu bila kuwapo kwa
uthibitisho wa tuhuma husika.
TEF inaendelea kuchukua hatua nyingine za ndani kuimarisha usimamizi
wa nidhamu na maadili kwa wahariri, na itaendelea kuchukua hatua dhidi
ya ukiukwaji wowote ule wa kitaaluma utakaofanywa katika vyombo vya
habari.
No comments:
Post a Comment