CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemkabidhi hundi
ya sh milioni 1.3, Celina Peter, mama wa mtoto Beatrice Shemtibuka,
anayesumbuliwa na matatizo ya moyo anayetakiwa kupelekwa India kwa
matibabu.
Hundi hiyo alikabidhiwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Katibu wa
CHADEMA wa Wilaya ya Arusha, Maltin Sarungi, ikiwa ni mchango wa
wanachama na wapenzi wa chama hicho kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo.
Sarungi alisema fedha hizo zilichangwa na wanachama kupitia mkutano wa
hadhara baada ya mama huyo kumueleza Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema, matatizo yanayomkabili mwanae.
Alifafanua kuwa mbunge akalazimika kulizungumzia suala hilo katika
mkutano huo na kuwaomba wanachama na wapenzi kumsaidia mama huyo ambapo
yeye kama mbunge aliahidi kusaidia tiketi ya kwenda India kwa matibabu
ya mtoto huyo.
Akizungumzia chanzo cha tatizo la mtoto wake, mama huyo alisema awali
alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kukosa sehemu ya haja kubwa na
kulazimika kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na
baada ya tatizo hilo kwisha akabainika ana tatizo la moyo.
Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha, Effata Nanyaro, alitoa wito
kwa serikali kujitahidi kuboresha sekta ya afya nchini ili kuwezesha
wenye matatizo kama hayo waweze kutibiwa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment