Clouds Media, jana walifungua mdomo kwa mara ya kwanza tangu Jaydee alipokuwa akiwarushia makombora kwa madai kuwa wamemfanyia mambo mabaya na kutaka kumuangamiza kimaendeleo.
Ruge Mutahaba.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Mutahaba alisema Jaydee amekuwa akilalamikia mambo mawili ambayo ni bendi ya Skylight na matangazo yake yaliyoshindwa kurushwa hewani japo alilipia sh 240,000.
Alisema suala hilo walilimaliza baada ya kumueleza kuwa redio yao
haiwezi kukataa matangazo, kwa kuwa ndiyo yanayowafanya waendelee kuwa
kinara katika suala zima la kuiendesha Clouds FM.
“Nilimwambia kamwe hatuwezi kukataa matangazo na kama kuna lolote
limefanyika, basi ni kwa bahati mbaya, ukizingatia kuwa tayari
alishafanya kazi nyingi pamoja na kupewa urahisi kwenye kazi zake kwa
kupitia Clouds FM.
“Pamoja na yote hayo, bado matusi na kejeli yaliendelea hasa katika
mitandao ya kijamii, jambo lililotufanya tuamue sasa kujibu japo hapo
kabla tuliamua kubaki kimya kwa ajili ya kulinda hadhi ya kazi zetu,”
alisema.
Kuhusu shutuma za kuitangaza zaidi Skylight, Ruge alisema, bendi hiyo
si mali ya Joseph Kusaga, mkurugenzi wao wala yeye, kama madai hayo
yanavyotolewa bila kufanya utafiti, isipokuwa ni mali ya Sebastian
Ndege.
“Kama kuna mvutano kati ya Machozi Bendi na Skylight, basi ni wa
kibiashara, maana wote wanalipa fedha za matangazo na kama chanzo ni
Jaydee kuporwa wanamuziki wake, hilo si jambo geni kwenye muziki.
Dada yangu Asha Baraka asingekuwa makini angelia sana, maana kila
bendi inayoanzishwa au kuendeshwa lazima ichukue wanamuziki kutoka
kwake, ukizingatia kuwa ni jambo la kawaida, hivyo tunamuomba Jaydee
atumie busara katika hili pamoja na kuumiza kichwa kupokea ushindani na
changamoto kama hizo za kuchukuliwa wanamuziki,” aliongeza Ruge.
Aidha, Ruge alisema Clouds FM ni redio ya watu binafsi, hivyo ina
utaratibu wake katika utendaji wa kazi, ikiwamo kuchagua nyimbo au
kuacha kupiga kama kuna mtu amekwenda kinyume, hasa wale wanaopita nje
na kuanza kuwatusi na kuwakejeli bila kukumbuka fadhila walizofanyiwa
kabla ya kuwa maarufu.
Pia alisema Clouds FM ipo tayari kufanya majadiliano ya wazi na mtu
yeyote mwenye hisia tofauti juu yao, huku ikiwataka wasanii waongeze
bidii katika kazi zao ili wasimlaumu mtu wanapoanguka na kuwapisha
wengine, maana muziki unaonekana ni wa kupokezana vijiti
No comments:
Post a Comment