Habari na Tanzania daima.
HALI ya mambo huenda ikavurugika tena mkoani Mtwara baada ya kuwepo
kwa taarifa za maandalizi ya mgomo na maandamano ya kudai kunufaika na
gesi.
Mwishoni mwa mwaka jana wananchi wa Mtwara walifanya maandamano
kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam
uliopangwa kutekelezwa na serikali.
Februari mwaka huu wananchi hao waliamua kufanya maandamano mengine
yaliyoambatana na vurugu ikiwemo kuchoma nyumba za viongozi wa CCM.
Baada ya kutokea matukio hayo, viongozi mbalimbali wa serikali,
akiwemo Waziri Mkuu, walikwenda kuzungumza na wananchi hao jinsi ambavyo
wangelinufaika na gesi hiyo.
Miongoni mwa ahadi walizopewa ni kuboreshwa kwa bandari ya Mtwara,
kujengwa kwa kiwanda cha saruji na uwanja wa ndege wa kisasa ambavyo
vitachangia kukua kwa uchumi wa mkoa huo.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa baadhi ya watu wamesambaza vipeperushi
mitaani kuwahamasisha wananchi kujiandaa kusikiliza na kuangalia hotuba
ya Wizara ya Nishati na Madini.
Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi, vipeperushi hivyo vinawataka
wasifanye shughuli yoyote siku bajeti hiyo itakaposomwa ili wajue hatima
ya gesi iliyoko mkoani mwao.
“Tuliambiwa leo bajeti ya Nishati na Madini itasomwa lakini baadaye
tunaambiwa itasomwa wiki ijayo…hapa watu wamejipanga kuifuatilia,”
alisema Nchiman Joseph.
Moja ya vipeperushi kilisomeka: “Zinduka kusini, wananchi kwa pamoja. JK ameamua kutumia nguvu kwenye suala la gesi.
“Kwa pamoja Mei 17, 2013 saa tano asubuhi tukusanyike kwenye vituo vya
runinga ili kusikiliza bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini; tutambue
vema sakata la gesi, sambamba na hilo tusitishe huduma zote za jamii
ikiwemo bodaboda, teksi, bajaji na magari ya abiria-zinduka Mtanzania!”
Tanzania Daima imedokezwa kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Linus
Sinzumwa, ameonekana katika kituo cha redio kiitwacho Pride FM
kuwatahadharisha wananchi kuhusu vipeperushi hivyo.
Kamanda huyo aliwaambia wananchi wasihofu juu ya usalama wao kwa kuwa
polisi imejipanga kuhakikisha vurugu zilizotokea huko nyuma hazitokei
tena.
Tanzania Daima iliwasiliana na Kamanda Sinzumwa ambaye alikiri kuna
taarifa za vipeperushi hivyo na kuwataka wananchi wavipuuzie.
“Ni kweli vipeperushi vipo ila hali ni shwari…, nyie mnataka kukuza
tu, nimeshatoa tahadhari na tutafanya udhibiti mkubwa sana,” alisema.
Nyumba za kulala wageni
Chanzo chetu cha taarifa kimedokeza kuwa nyumba ya kulala wageni
zilikuwa na wegeni wengi ambao wengine wakisadikiwa ni askari kutoka
makao makuu ya jeshi la polisi.
Mmoja wa wananchi alizungumza na gazeti hili kwa simu alisema: “sisi
wananchi wa Mtwara tumekuwa gizani kwa kipindi kirefu bila kujua lengo
la serikali katika suala la gesi ambayo itachimbwa huku tumekubaliana
na masuala ambayo tuliyataka yatolewe ufafanuzi ambapo serikali
haikufanya hivyo.”
Aliongeza kuwa wananchi wanataka kuona mambo waliyokubaliana na
serikali katika mikutano mbalimbali yanatekelezwa kwa kuwekwa katika
bajeti hiyo.
“Sisi hatuna ugomvi na serikali; tunachotaka ni kuona utekelezaji wa
masuala tuliyokubaliana yanakuwepo katika bajeti ambayo kwetu
yatatuwezesha kuendelea kiuchumi na sio kuonekana wazalishaji lakini
wananufaika wengine,” alisema Mpendela.
Baadhi ya wananchi hao walilalamika kuwa suala la gesi linapelekwa
kisiasa huku wananchi wakiwa njia panda bila kujua ni maslahi gani
watakayonufaika nayo.
Shura ya Maimamu
Viongozi wa Shura ya Maimamu ni miongoni watu waliofanya mazungumzo na kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara juu ya tisho la vurugu.
“Sisi tumefanya vikao sio leo tangu juzi, kamanda wa polisi alituita
ingawa yeye bado ni mgeni alitaka tujadili suala la amani ya mji wa
Mtwara na dhana ya utii wa sheria bila shuruti katika kikao hicho
tuliunda kamati ya watu 10, Wakristo watano na Waislamu watano.
“Leo alituita ili tujadili ni nani anahusika na vipeperushi hivi. Kwa
hiyo tumetoa tamko kuwa kesho wananchi waendelee na shughuli zao kwani
siku ya kesho sio ya kujadili Bajeti ya Nishati na Madini, tumemkabidhi
kamanda wa polisi wa mkoa aende kwenye vyombo vya habari kuisoma ili
awaarifu wananchi,” alisema mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo.
Kiongozi huyo alitaka elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili mtoaji wa vipeperushi hivyo ajulikane.
“Hatutaki vurugu zitokee hii leo,…. maana wengine wanaweza wakaleta
dhana ya udini ikaonekana Waislamu wametengeneza au Wakristo wanatumia
mwanya huo kuharibu Ijumaa.
“Sisi Waislamu na Wakristo tulio katika tume hiyo tunawaasa wananchi wasifanye hivyo.
No comments:
Post a Comment