Nyaraka za
barua za mawasiliano kuhusu maendeleo ya jalada la kesi ya mauaji ya
Padri Evarist Mushi inayomkabili Omar Mussa Makame, zimevuja baada ya
wakili anayemtetea mtuhumiwa huyo kuziwasilisha mahakamani jana mjini
Zanzibar. Barua
hizo pamoja na taarifa za kikao kilichofanyika Aprili 4 mwaka huu
kujadili jalada la uchunguzi wa kesi hiyo inadaiwa kiliwahusisha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Othman Masoud
Othman, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim,
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa na Naibu
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Upelelezi, (DDCI) Yusuph Ilembo.
Wakili wa
upande wa utetezi Abdallah Juma Mohamed alitoa taarifa hizo wakati
akipinga hoja ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Abdallah Issa Mgongo,
baada ya kuiomba Mahakama Kuu kuahirisha shauri la kesi hiyo kwa madai
upelelezi bado haujakamilika.
Wakili huyo
alisema kwamba amefanikiwa kupata barua yenye kumbukumbu namba
BUB/P89/VOLV/54 ya Machi 25 mwaka huu, ambayo imeandikwa na Inspekta wa
Jeshi la Polisi Suleiman Suleiman kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa
wa Mjini Magharibi ambayo ilikuwa ikimtaka mkuu wa upelelezi kulipitia
kwa kina jalada la uchunguzi na kumtaarifu kuwa mtuhumiwa amehojiwa na
ametambuliwa katika gwaride maalum.
Alisema
barua hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari 'Kuua kwa makusudi Padri
Evarist Mushi’ baadae jalada hilo lilipelekwa kwa Naibu Mkurugenzi wa
Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar kabla ya kuwasilishwa katika Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim.
Wakili
Abdallah Juma Mohamed alisema kwa mujibu wa barua hiyo ambayo nakala
yake aliikabidhi mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mkusa Isaac
Sepetu, Inspekta Suleiman alisema amewasilisha jalada hilo kwa ajili ya
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani kwa
mtuhumiwa huyo.
Alisema
kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wake, Machi 26 mwaka huu, majumuisho ya
ushahidi wote uliopatikana yalifanyika na jalada la kesi kupelekwa kwa
DPP, ambapo Aprili 4 Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
Zanizbar, Yusuph Ilembo alikula kiapo mbele ya Mrajis wa Mahakama Kuu
cha kuthibitisha kukamilika kwa uchunguzi wa jalada la kesi hiyo.
Alisema
kimsingi hakubaliani na hoja ya mteja wake kuendelea kubaki mahabusu
hasa kwa kuzingatia Machi 25, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya
Mwanakwerekwe Janeth Sekiola alipokea ombi la Jeshi la Polisi la kuomba
kuongezewa muda wa kuendelea kumhoji mtuhumiwa na kutoa kibali hicho.
Wakili huyo
alisema kitendo cha mteja wake kuendelea kubakia mahabusu kutokana na
ushahidi wa kesi hiyo kutokamilika, kinakwenda kinyume na kifungu cha
14(1)(2) cha katiba ya Zanzibar kinachozungumzia haki ya mtu kuwa huru
na kuishi kama mtu huru.
Hata hivyo,
Mwanasheria wa Serikali, Abdallah Issa Mgongo alipinga hoja hizo na
kuieleza mahakama kuwa kesi ya msingi haiwezi kuanza kusikilizwa kabla
ya kukamilika kwa ushahidi, kwa vile Jamhuri ni watu na upande wa
mashtaka ili kuhakikisha haki ya kisheria inatendeka mahakamani.
"Mheshimiwa
Jaji, DPP hana nia ya kumkandamiza wala kumuonea mshtakiwa, lengo letu
ni kuhakikisha upelelezi unajitosheleza na kuuleta mbele ya mahakama
yako, ili uweze kuusikiliza na kuutolea uamuzi" alisema Abdallah Issa
Mgongo.
Kwa upande
wake, Jaji Mkusa Isaac Sepetu aliliahirisha shauri hilo hadi Mei 21
mwaka huu, ambapo atatoa maamuzi kuhusu hoja zilizowasilishwa na pande
zote mbili, ikiwemo suala la mtuhumiwa huyo kuachiwa huru kutokana na
upande wa mashataka kuchelewa kuwasilisha ushahidi mahakamani.
habari naMWINYI SADALLAH
chanzo -NIPASHE
No comments:
Post a Comment