MKURUGENZI wa Kampuni ya Lino International Agency na mratibu
wa shindano la urembo la Redd’s Miss Tanzania 2013, Hashim Lundenga,
ameishukuru jamii kwa kuyaunga mkono mashindano hayo hali inayosababisha
kuwa na ubora na kuliongezea heshima taifa.
Lundenga alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokutana na
waandishi wa habari kuelezea mwelekeo wa shindano hilo ambalo kwa sasa
lipo hatua ya vitongoji na wilaya ambayo yatakamilika mwishoni mwa Mei.
“Nichukue fursa hii kuwajulisha wadau wa sanaa ya urembo kuwa hatua ya
ngazi ya vitongoji na wilaya yalishaanza kwa nchi nzima na tayari
baadhi ya maeneo wameshamaliza na maeneo mengine yakitarajia kumaliza
mwisho wa mwezi huu, tunashukuru kwa kuyapokea,” alisema Lundenga.
Alisema kutokana na mwamko huo, kutakuwa na mikoa 24 inayofanya
mashindano; kanda 11, vyuo vya elimu ya juu 17, wilaya 18, huku vituo
vya Mkoa wa Dar e Salaam vikiwa 11, vyote kwa pamoja vinafanya idadi ya
vituo zaidi ya 80.
Kwa hatua hiyo, Lundenga alisema baada ya kumalizika kwa mashindano
hayo ya awali, hatua ya kanda itafuata katikati ya Juni na kuingia
katika hatua inayofuata.
Lundenga amewashukuru wazazi na walezi ambao wamewaruhusu watoto wao
wasichana kujitokeza kwa wingi katika ushiriki wa shindano hilo.
Kwa upande wake Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original, Victoria
Kimaro, alisema kupitia kinywaji chao bora hapa nchini cha Redd’s,
kimedhamiria kuwapo kwa ubora na kuendelea kutoa udhamini kwa ngazi
zote.
Lundenga amewasihi wadau kuendelea kukiunga mkono kinywaji hicho ili kuweza kupata nguvu ya kuwaletea burudani.
Fainali hizo kwa leo zinatarajia pia kufanyika katika sehemu
mbalimbali ikiwamo Redd’s Miss Moshi Mjini, Redd’s Miss Kibaha, Redd’s
Chuo cha Ustawi wa Jamii, Redd’s Miss Ubungo na Redd’s Miss Mzizima.
No comments:
Post a Comment