SIKU chache baada ya serikali kutangaza uamuzi wa kuyafuta na
kupitia upya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2012, wadau wa
sekta ya elimu wameupinga kwa madai umetolewa kwa kukurupuka.
Wadau hao wameitaka serikali iache kukurupuka katika jambo hilo kwa
kuwa sababu za msingi za kufeli kwa wanafunzi hao zinafahamika ila
hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa hadi sasa.
Muungano wa asasi tano za kiraia uliowakilishwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa HakiElimu Elizabeth Missokia, ndiyo uliotoa tamko hilo jana
jijini Dar es salaam ulipokuwa ukizungumza na waandishi wa habari.
Asasi zinazounda muungano huo ni Hakielimu, Policy forum, Sikika,
TenMet na TGNP ambazo zimeitaka serikali iache visingizio vya kushuka
kwa elimu bali iwekeze kikamilifu katika sekta ya elimu.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Missokia alisema hakukuwa na haja ya
kufuta matokeo hayo na kuyaangalia upya bali kufanya maboresho katika
sekta ya elimu ndiyo jambo muhimu zaidi.
Missokia alisema kabla ya serikali kutoa uamuzi huo ilitakiwa kuweka
wazi mapendekezo ya
Tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, iliyoundwa
kuchunguza matokeo hayo ili wadau wa elimu wapate fursa ya kuona sababu
zilizochangia kushuka kwa ufaulu katika mitihani hiyo.
“Kwa kufuta matokeo hayo bila wadau kujua sababu na kutoa mchango wao
inawaaminisha Watanzania kwamba sababu nyingine hata kama zipo
ziliathiri kwa kiwango kidogo matokeo hayo na suala la upangaji wa
madaraja kuonekana ni sababu kubwa zaidi kuliko nyingine,” alisema
Missokia.
Alisema hiyo sio sababu kwani matokeo ya kidato cha nne yaliyopita
hayakuwa mazuri huku akiyataja ya mwaka 2009 kuwa yalikuwa na asilimia
27.5 ya watahiniwa waliopata daraja sifuri; mwaka 2010 sifuri walikuwa
asilimia 49.6; na mwaka 2011 asilimia 46.4 walipata daraja sifuri ambayo
ni matokeo mabaya pia.
Alisema kwa mtiririko huo wa matokeo ni lazima kulikuwa na sababu
kubwa zaidi iliyochangia kushuka kwa ufaulu na kwamba hakuna uhusiano
wa moja kwa moja kati ya kubadili utaratibu wa kupanga matokeo na
ufaulu duni wa 2012.
Ilielezwa sababu nyingine ni kutokuwa na walimu wa kutosha hasa kwa
masomo ya sayansi, shule kuwa na upungufu mkubwa wa vitabu na vifaa
mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia.
Alizitaja sababu nyingine kuwa ni bajeti ya maendeleo shuleni kuwa
ndogo, ruzuku mashuleni kufika ikiwa pungufu na wakati mwingine ikiwa
imechelewa, mihtasari ya kufundishia ina mkanganyiko mkubwa na huku
mtaala mpya wa mwaka 2005 ukiwa mgeni kwa walimu walio wengi.
“Msingi mbovu wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya
mawasiliano darasani; walimu kutokuwa na hamasa ya kufundisha kutokana
na madai ya muda mrefu na kufanya kazi katika mazingira magumu sambamba
na kukosekana kwa mafunzo kazini ya kuwaimarisha katika ufundishaji wao;
na hamasa ndogo miongoni mwa wazazi katika kufuatilia malezi ya watoto
wao,” alisema Missokia.
Hata hivyo alieleza kuwa kuandaliwa upya kwa matokeo hayo, serikali
inatakiwa ikumbuke kuna athari mbalimbali ambazo zitatokea ikiwa ni
pamoja na baadhi ya wanafunzi ambao walijiua baada ya kupata matokeo
mabaya sasa endapo watatoka na kupata alama za juu nani atakayetakiwa
kuwajibishwa kwa hilo.
Pia kuna baadhi ya wanafunzi na wazazi wameshafanya maamuzi
mbalimbali, pamoja na waliokata tamaa na wamepata madhara makubwa
kisaikolojia na wengine kukubali kurudia mitihani na kuhoji serikali
itatoa fidia gani.
Pia waliishukia NECTA kutokana na kukanusha kutumika kwa utaratibu
mpya wa upangaji wa madaraja huku wakihoji kuwa taasisis hiyo
iliwadanganya Watanzania.
Asasi pia zilieleza kwa kuwa serikali imeamua kufuta matokeo hayo na
hatimaye kupangwa upya kwa utaratibu wa mwaka 2011 zilishauri zoezi hilo
kufanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wadau wengine wa elimu ili
kujiridhisha na uhalali wa alama za wanafunzi zitakazokuwa
zinarekebishwa na siyo kufanya uchakachuaji katika njia za urekebishaji
na upangaji wa matokeo katika madaraja.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment